22. Tunapozozana katika jambo la ´Aqiydah

Moja katika sifa za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuwa anahukumu kati ya watu katika yale waliyotofautiana kwayo – na anahukumu kati yao kwa Qur-aan:

وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ

“Wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Allaah na wala usifuate matamanio yao.”[1]

إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّـهُ

”Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili uhukumu kati ya watu kwa aliyokuonyesha Allaah.”[2]

Miongoni mwa mambo makubwa ambayo kumetokea mizozo kati ya watu ni mambo yanayohusu majina na sifa za Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alihukumu suala hilo na akabainisha kuwa majina na sifa za Allaah (´Azza wa Jall) ni sifa za kikweli – na kwa hukumu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio ya haki:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[3]

Bi maana mnapozozana katika jambo lolote lile, kubwa na dogo. Jambo kubwa ambalo watu wamezozana kwalo ni jambo la ´Aqiydah. Ni lazima mizozo ihukumiwe kwa Qur-aan na Sunnah, na si katika mantiki, elimu ya falsafa na fahamu za watu. Wale wanaofupisha magomvi ya kiuchumi katika dini na wanapuuza kipengele cha ´Aqiydah hawako juu ya lolote. Wameacha msingi na wakashikilia tawi. Jambo muhimu zaidi ambalo ni wajibu kuhukumiwa na Qur-aan na Sunnah ni magomvi katika jambo la ´Aqiydah. Tunapotofautiana katika ´Aqiydah, basi tunapaswa kurejea katika Qur-aan na Sunnah. Tunapotofautiana katika majina na sifa za Allaah, basi tunapaswa kurejea katika Qur-aan na Sunnah. Tunapotofautiana katika mambo ya ´ibaadah, basi tunapaswa kurejea katika Qur-aan na Sunnah. Ikiwa ´ibaadah hiyo imetajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah, basi ni sahihi. Ikiwa haikutajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah, basi ni Bid´ah:

”Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, basi atarudishiwe mwenyewe.”[4]

[1] 5:49

[2] 4:105

[3] 4:59

[4] Muslim (1718).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 29/07/2024