22. Tafsiri ya baadhi ya istilahi za ´Aqiydah zilizotajwa na Ahl-us-Sunnah

Swali 22: Katika vitabu vya Ahl-us-Sunnah, kunatajwa baadhi ya isitilahi kama vile kujitolea (الالتزام), kujizuilia ( الامتناع) na kufuru ya kupuuza (كفر الإعراض). Nini maana ya istilahi hizi?

Jibu: Maana yake ni kulazimiana na hukumu za Shari´ah kwa kufanya yale ambayo Allaah ameamrisha na kujiepusha na yale ambayo Allaah amekataza.

Maana ya kujizuilia ni kukataa kutekeleza yale ambayo Allaah ameamrisha. Hili linahitaji maelezo zaidi:

1 – Ikiwa mtu anajizuilia na jambo ambalo kuliacha kwake ni ukafiri, basi mtu huyo anahukumiwa kuwa kafiri.

2 – Ikiwa mtu anajizuilia na jambo ambalo kuliacha kwake hakufikii kiwango cha ukafiri, basi mtu huyo anakuwa mtenda dhambi.

Miongoni kwa ukafiri wa kujizuilia ni ni kitendo cha Ibliys kukataa kumsujudia Aadam. Amesema (Ta´ala):

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ

”Kumbuka Tulipowaambia Malaika: ”Msujudieni Aadam”, wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri.”[1]

Ukataaji wa Ibliys ni kufuru.

Kufuru ya kupuuza ni kuipuuza dini ya Allaah kwa namna ya kwamba mtu hajifunzi nayo na wala hamwabudu Allaah.

[1] 02:34

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 52
  • Imechapishwa: 08/01/2026