Suala la pili: Swawm iliyopendekezwa

Miongoni mwa hekima na rehema Zake juu ya waja Wake ni kuwajaalia kuwa na ´ibaadah zilizopendekezwa ambazo zinafanana na zile za faradhi. Yote hayo ni kwa sababu ya ziada katika ujira na thawabu kwa watendaji na kuunga upungufu na kasoro zinazoweza kujitokeza katika zile ´ibaadah za faradhi. Tayari tumekwishatangulia kusema kwamba ´ibaadah za sunnah zitakamilisha zile ´ibaadah za faradhi siku ya Qiyaamah. Siku ambazo zimependekezwa kufunga ni zifuatazo:

1- Kufunga siku sita za Shawwaal. Abu Ayyuub al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yule mwenye kufunga Ramadhaan kisha akaifuatizia [siku] sita za Shawwaal, basi ni kama amefunga mwaka mzima.”[1]

2- Kufunga siku ya ´Arafah kwa ambaye hayuko hajj. Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Funga ya siku ya ´Arafah nataraji kwa Allaah kunifutia [madhambi ya] mwaka wa kabla yake na mwaka wa baada yake.”[2]

Kwa mwenye kuhiji haikusuniwa kwake kufunga siku ya ´Arafah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikula siku hiyo na huku watu wakimtazama. Jengine ni kwamba jambo hilo linamtia nguvu za kufanya ´ibaadah na kuomba du´aa katika siku hiyo yule mwenye kuhiji.

 3- Swawm ya siku ya ´Aashuuraa´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu funga ya siku ya ´Aashuuraa´ ambapo akasema:

“Nataraji kwa Allaah atanisamehe [madhambi ya] mwaka wa kabla yake.”[3]

Imependekezwa kwa mtu kufunga pia siku moja kabla yake au baada yake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Lau nitabaki mpaka mwaka ujao basi nitafunga siku ya tisa.”[4]

“Fungeni siku moja kabla yake au siku moja baada yake – jitofautisheni na mayahudi.”[5]

[1] Muslim (1164).

[2] Muslim (1162).

[3] Muslim (1162).

[4] Muslim (1133).

[5] Ahmad (01/241) na Ibn Khuzaymah (2095).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 162
  • Imechapishwa: 01/05/2020