22. Kuogopa kutumbukia katika shirki na kuhusu kama ujinga ni udhuru

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

2 – Faida ya pili: Umefaidika pia [kuwa na] khofu kubwa. Ukijua ya kwamba mtu anaweza kukufuru kwa neno analolitoa mdomoni mwake, na pengine amelisema na yeye ni mjinga [hajui], hata hivyo hapewi udhuru kwa ujinga..

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Faida ya pili: “Umefaifika pia [kuwa na] khofu kubwa… ”

Bi maana usije kutumbukia ndani ya yale waliyotumbukiaemo watu hawa wajinga kwa kutoelewa maana yake na ukhatari mkubwa wa jambo hilo.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… hata hivyo hapewi udhuru kwa ujinga… “

Hapa tutafanyia taaliki maneno ya mtunzi (Rahimahu Allaah) ifuatavyo:

1 – Sifikirii kuwa Shaykh (Rahimahu Allaah) haonelei ujinga kuwa ni udhuru. Isipokuwa ikiwa inahusiana mtu kutotaka kujifunza. Mfano wa hilo ni kama mtu kusikia haki na kupuuza kujifunza. Mtu kama huyu hapewi udhuru kwa ujinga wake. Sababu ya mimi kutofikiria hivi kutoka kwa Shaykh, ni kwa sababu ana maneno mengine ambapo yanafahamisha kuwa mtu anapewa udhuru kutokana na ujinga. Aliulizwa (Rahimahu Allaah) swali anapigana vita kwa kitu gani na kwa kipi anamkufurisha mtu kwacho? Akajibu:

“Nguzo tano za Uislamu. Ya kwanza ni shahaadah halafu kunakuja nguzo nne zingine. Kuhusiana na hizo nne, hatuonelei yule mwenye kuzithibitisha na akaziacha kutokana na uvivu kuwa ni kafiri, hata kama tutampiga vita. Wanachuoni wametofautiana juu ya yule mwenye kuziacha kutokana na uvivu pasi na kuzikanusha. Wanachuoni wote wamekubaliana juu ya kwamba yule mwenye kuacha shahaadah ni kafiri. Na sisi pia huo ndio msimamo wetu. Hali kadhalika tunaonelea kuwa ni kafiri akikanusha baada ya kusimamikiwa na hoja. Kwa ajili hiyo tunasema kuwa tuna aina nne ya maadui:

1 – Yule mwenye kujua kuwa Tawhiyd ndio dini ya Allaah na ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akajua kuwa ni shirki kuwa na imani juu ya mawe, miti na watu, kama wanavyofanya watu wengi, na kwamba Allaah alimtuma Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuyakataza hayo na kuwapiga vita watu hawa ili aabudiwe Allaah peke Yake, pamoja na hivyo asijali Tawhiyd, kujifunza nayo, kuingia ndani yake na asiache shirki, kwamba ni kafiri. Tunapigana vita na mtu huyu kwa sababu ya ukafiri wake. Kwa sababu mtu huyu ameijua dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kuifuata na amejua shirki ni kitu gani na hataki kuiacha. Mambo ni namna hii hata kama hatoichukia dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala wale wenye kuingia katika dini hiyo. Isitoshe hasifu shirki wala haiwapambii nayo watu.

2 – Mwenye kuyajua yote haya lakini akaitukana dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – pamoja na kudai kuwa anaitendea kazi – na anawasifu wale wenye kumuabudu Yuusuf, al-Ashqar, Abu ´Aliy na al-Khadhwir kutoka Kuwait na kuonelea kuwa wao ni bora kuliko wale wenye kumuabudu Allaah peke Yake na wamejitenga na shirki. Huyu ni mbaya zaidi kuliko huyo wa kwanza. Amesema (Ta´ala):

فَلَمَّا جَاءَهُم مَّا عَرَفُوا كَفَرُوا بِهِ ۚفَلَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الْكَافِرِينَ

“Yalipowajia yale waliyokuwa wakiyatambua waliyakanusha, basi laana ya Allaah iwe juu ya wakanushaji.” (02:89)

Vilevile Allaah amesema juu ya mtu kama huyo:

وَإِن نَّكَثُوا أَيْمَانَهُم مِّن بَعْدِ عَهْدِهِمْ وَطَعَنُوا فِي دِينِكُمْ فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ ۙ إِنَّهُمْ لَا أَيْمَانَ لَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَنتَهُونَ

“Na wakivunja viapo vyao baada ya ahadi yao na wakatukana dini yenu, basi wapigeni vita viongozi wa ukafiri. Hakika viapo vyao havina maana. [Piganeni nao] ili wapate kukoma.” (09:12)

3 – Yule mwenye kujua Tawhiyd, anaipenda, anaifuata na anaijua shirki na anaichukia, lakini anamchukia yule mwenye kuingia katika Tawhiyd na anampenda yule mwenye kubaki katika shirki. Mtu huyu ni kafiri. Amesema (Ta´ala) juu ya mtu kama huyu:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

“Hivyo kwa sababu wao wamechukia yale aliyoteremsha Allaah, basi akayaporomosha matendo yao.” (47:09)

4 – Ambaye hana sifa hata moja katika hizi. Lakini watu wa mji wake wanaonyesha uadui wa waziwazi kwa watu wa Tawhiyd na wakati huohuo wanawaonyesha mapenzi washirikina. Wanajitahidi kupambana nao. Mtu huyu anapewa udhuru kwa sababu kuna uzito kwake kwa yeye kuuacha mji wake. Anawapiga vita watu wa Tawhiyd bega kwa bega pamoja na watu wa mji wake na akapambana vita kwa mali na nafsi yake. Mtu huyu pia ni kafiri. Wakimuamrisha kuacha kufunga Ramadhaan, aachane nao ikiwa ndio njia pekee ya kuweza kufunga. Wakimuamrisha kumuoa mke wa baba yake, aachane nao ikiwa ndio njia pekee. Hata hivyo ni jambo la khatari sana kuafikiana nao kupigana vita bega kwa bega pamoja na wao kwa nafsi na mali yake kwa vile wanakusudia kuitokomeza dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu huyu pia ni kafiri. Allaah amesema juu ya mtu kama huyu:

سَتَجِدُونَ آخَرِينَ يُرِيدُونَ أَن يَأْمَنُوكُمْ وَيَأْمَنُوا قَوْمَهُمْ

“Mtawakuta wengine wanaotaka kupata amani kwenu na kupata amani kwa watu wao.” (04:91)

Haya ndio tunayosema.

Ama kuhusu uongo na uzushi ya kwamba tunawakufurisha watu kwa njia ya jumla, tunamuwajibishia kuhajiri kuja kwetu kwa wale ambao wanaweza kuidhihirisha dini yao na kwamba tunawakufurisha wale wote ambao hawakufurishi na kuwapiga vita wengine, huu ni uongo kabisa. Ni njia ya kuwazuia watu na dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Alalahu ´alayhi wa sallam). Ni vipi tutamkufurisha mtu ambaye hamshirikisha Allaah endapo hatohajiri kuja kwetu na kuwakufurisha na kuwapiga vita wengine, ikiwa hatuwakufurishi wale wenye kuabudu masanamu kwenye kaburi la ´Abdul-Qaadir, Ahmad al-Badawiy na makaburi ya watu mfano wao kwa sababu ya ujinga wao na kwa sababu hakuna mwenye kuwakumbusha?

سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ

“Utakasifu ni Wako – Huu ni usingiziaji mkubwa mno!” (24:16)

Uhakika wa mambo ni kuwa tunakufurisha kwa sampuli zile nne kwa sababu zinapingana na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah amrehemu mtu mwenye kuitazama nafsi yake na kutambua kuwa atakuja kusimama mbele ya Allaah ambaye Kwake ndiko kuna Pepo na Moto.

Swalah na amani zimwendee Muhammad, kizazi  chake na Maswahabah zake[1].

Ukamilisho:

Tofauti juu ya suala la ujinga ni udhuru au sio udhuru, ni kama masuala mengine yote ya ki-Fiqh na ya Ijtihaad. Huenda wakati mwingine ikawa ni tofauti ya kimatamshi kwa ajili ya kutekeleza hukumu fulani kwa mtu maalum. Kwa msemo mwingine kukawa kuna maafikiano juu ya kwamba matamshi fulani, kitendo fulani au kuacha jambo fulani ni kufuru. Lakini ina maana kuwa ni sahihi kumtekelezea hukumu hii mtu maalum kwa sababu inahitajia awe amewekewa wazi na kusiwepo kizuizi? Au haiwezekani kufanya hivo kwa sababu kunakosekana baadhi ya mambo au bado kuna vizuizi fulani? Yote hayo yanategemea kwamba ujinga juu ya kufuru umegawanyika aina mbili:

1 – Mjinga huyo awe ni mtu ambaye anafuata dini nyingine isiyokuwa Uislamu au hafuati dini yoyote kwa njia ya kwamba hajapatapo kamwe kufikiria kuwa hali aliyomo inaenda kinyume na dini fulani. Mtu kama huyu atatekelezewa hukumu za dhahiri katika dunia hii. Kuhusiana na hali yake huko Aakhirah, inajua Allaah (Ta´ala). Maoni sahihi zaidi ni kuwa, atapewa mtihani huko Aakhirah kwa kile ambacho Allaah (´Azza wa Jall) atataka. Allaah ndiye ajuaye zaidi ni kipi wangefanya. Lakini tunajua kuwa hatoingia Motoni isipokuwa kwa madhambi. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا

“Na Mola wako hamdhulumu yeyote.” (18:49)

Tumesema kuwa atatendewa hukumu za dhahiri duniani, ambazo ni hukumu za makafiri, ni kwa sababu hafuati dini ya Uislamu na ndio maana hatuwezi kumhukumu kwa hukumu zake. Tunasema kuwa atapewa mtihani huko Aakhirah kwa sababu kuna mapokezi mengi yenye kusema hivo. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ameyataja katika kitabu chake “Twariyq-ul-Hijratayn” pindi alipokuwa akizungumzia aina ya nane kuhusu watoto wa washirikina.

2 – Mjinga anayejinasibisha na Uislamu. Ameishi katika ukafiri huu na wakati huohuo hajapatapo kufikiria kuwa anaenda kinyume na Uislamu. Isitoshe hakuna yeyote aliyemkumbusha juu ya hilo. Mtu kama huyu atahukumiwa kwa hukumu za Uislamu kwa dhahiri. Kuhusiana na hali yake huko Aakhirah, Allaah (´Azza wa Jall) ndiye anayejua zaidi itavyokuwa. Dalili ya hilo ni Kitabu, Sunnah na maneno ya wanachuoni. Kuhusiana na Kitabu, maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا

“Na Hatukuwa wenye kuadhibu yeyote mpaka Tuwapeleke Mitume.” (17:15)

وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَىٰ حَتَّىٰ يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولًا يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا ۚ وَمَا كُنَّا مُهْلِكِي الْقُرَىٰ إِلَّا وَأَهْلُهَا ظَالِمُونَ

“Na Mola wako hakuwa Mwenye kuangamiza miji mpaka apeleke katika miji mikuu yake Mtume awasomee Aayah Zetu. Na Hatukuwa Wenye kuangamiza miji isipokuwa watu wake wawe madhalimu.” (28:59)

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume hali ya kuwa ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya [kuletwa] Mitume.” (04:165)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ۖ فَيُضِلُّ اللَّـهُ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ

“Na Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa kwa lugha ya watu wake ili awabainishie. Basi Allaah humpotoa amtakaye na humuongoza amtakaye.” (14:04)

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِلَّ قَوْمًا بَعْدَ إِذْ هَدَاهُمْ حَتَّىٰ يُبَيِّنَ لَهُم مَّا يَتَّقُونَ

“Na haiwi kwa Allaah awapotoze watu baada ya kuwa amewaongoa mpaka awabainishie ya kujikinga nayo.” (09:115)

وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ أَن تَقُولُوا إِنَّمَا أُنزِلَ الْكِتَابُ عَلَىٰ طَائِفَتَيْنِ مِن قَبْلِنَا وَإِن كُنَّا عَن دِرَاسَتِهِمْ لَغَافِلِينَ أَوْ تَقُولُوا لَوْ أَنَّا أُنزِلَ عَلَيْنَا الْكِتَابُ لَكُنَّا أَهْدَىٰ مِنْهُمْ ۚ فَقَدْ جَاءَكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ

“Na Kitabu hiki Tumekiteremsha kilichobarikiwa; basi kifuateni na muwe na mumche ili mpate kurehemewa. [Tumewateremshia Kitabu] msije mkasema: “Hakika Kitabu kimeteremshwa juu ya makundi mawili [mayahudi na manaswara] kabla yetu; lakini tulikuwa bila ya shaka tumeghafilika kuhusu waliyokuwa wakiyasoma” – au mkaseme: “Lau tungeliteremshiwa Kitabu basi, bila shaka tungelikuwa waongofu zaidi kuliko wao.” Kwa hakika imekwishakufikieni hoja ya wazi kutoka kwa Mola wenu na mwongozo na  rehema.” (06:155-157)

Kuna Aayah nyingi zinazofahamisha kuwa hoja haisimami isipokuwa baada ya ujuzi na ubainifu.

Ama kuhusu Sunnah, imepokelewa katika “as-Swahiyh” ya Muslim[2] kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mkononi Mwake! Hakuna yeyote katika ummah huu atayesikia kuhusu mimi, si myahudi wala mnaswara, halafu akafa bila ya kuamini yale niliyotumwa kwayo isipokuwa atakuwa katika watu wa Motoni.”

Kuhusu maneno ya wanachuoni, amesema [Ibn Qudaamah] katika “al-Mughniy”[3]:

“Ama yule asiyejua uwajibu kwa sababu ni muislamu mpya au amekulia katika mji usiokuwa wa Kiislamu au jangwani ambapo ni mbali na mahali kunakoeshi watu na wanachuoni, hatohukumiwa ukafiri.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Majmuu´-ul-Fataawaa”[4]:

“Mimi ni miongoni mwa watu wanaokataza vibaya sana kumpachika mtu ukafiri, mtenda dhambi na mtenda maasi. Wanaokaa na mimi wanajua hili. Isipokuwa tu ikiwa mtu anajua kuwa mtu huyo amesimamikiwa na hoja kutoka katika Ujumbe unaofanya yule mwenye kwenda nao kinyume anakuwa kafiri, mtenda dhambi au mtenda maasi. Mimi ninathibitisha kuwa Allaah (Ta´ala) amesamehe makosa ya ummah huu. Makosa haya yanajumuishwa ya kimaneno na ya kimatendo. Salaf daima waliendelea kujadiliana mengi katika mambo haya. Pamoja na hivyo hakuna yeyote aliyempachika mwingine ukafiri, utenda dhambi nzito na utenda maasi.”

Halafu akasema:

“Nilikuwa nikibainisha baadhi ya mapokezi kutoka kwa Salaf na maimamu ambapo wamempachika ukafiri mwenye kusema kadhaa na kadhaa na kwamba ni haki. Lakini, inatakiwa kwa mtu kutofautisha kati ya isiyofungamana na mtu maalum.”

Kisha akasema:

“Kumkufurisha mtu ni miongoni mwa makemeo. Hata kama maneno yanaweza kuwa na maana ya kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini ni lazima kutambua kuwa kuna uwezekano mtu huyo ndiye punde ameingia katika Uislamu au amekulia mbali jangwani. Mtu kama huyu asikufurishwe kwa kile alichokikanusha, mpaka pale ataposimamishiwa hoja. Hali kadhalika inaweza kuwa inahusiana na mtu ambaye hajasikia Maandiko hayo. Vilevile anaweza kuwa ameyasikia pasi na kuonelea kuwa yamethibiti au yamepingana na kitu kingine, jambo lenye kufanya akayapindisha maana ijapokuwa itakuwa ni makosa.”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab amesema[5]:

“Kuhusiana na kukufurisha, mimi namkufurisha tu yule ambaye ameitambua dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baada ya hapo akaitukana, akawazuia watu nayo na kuwafanyia uadui wale wenye kuitendea kazi. Mtu kama huyu ndiye ambaye ninamkufurisha.”

Katika ukurasa 66 amesema:

Ama kuhusu uongo na uzushi ya kwamba tunawakufurisha watu kwa njia ya jumla, tunamuwajibishia kuhajiri kuja kwetu kwa wale ambao wanaweza kuidhihirisha dini yao na kwamba tunawakufurisha wale wote ambao hawakufurishi na kuwapiga vita wengine, huu ni uongo kabisa. Ni njia ya kuwazuia watu na dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Alalahu ´alayhi wa sallam). Ni vipi tutamkufurisha mtu ambaye hamshirikisha Allaah endapo hatohajiri kuja kwetu na kuwakufurisha na kuwapiga vita wengine, ikiwa hatuwakufurishi wale wenye kuabudu masanamu kwenye kaburi la ´Abdul-Qaadir, Ahmad al-Badawiy na makaburi ya watu mfano wao kwa sababu ya ujinga wao na kwa sababu hakuna mwenye kuwakumbusha?

Ikiwa hivi ndivo kinavopelekea Kitabu, Sunnah na maneno ya wanachuoni, basi kadhalika ndivo inavyopelekea hekima, upole na huruma ya Allaah (Ta´ala). Hamuadhibu yeyote mpaka amuonyeshe dalili. Akili haiwezi kujitosheleza yenyewe kujua zile haki alizowajibisha Allaah (Ta´ala). Ingelikuwa inaweza kufanya hivo, basi hoja isingelisimama kwa kutumwa Mitume.

Msingi unasema yule mwenye kujinasibisha na Uislamu ni muislamu midhali dalili za Kishari´ah hazijathibitisha kinyume chake. Haijuzu kuchukulia usahali kumkufurisha, kwa sababu kitendo hicho kina dhambi mbili kubwa:

1 – Kumsemea uongo Allaah (Ta´ala) katika hukumu Yake. Vilevile ni kumsemea uongo yule muhukumiwaji kwa manasibisho kama hayo.

Ama kuhusiana na la kwanza ni jambo liko wazi kwa vile anamkufurisha yule ambaye hakukufurishwa na Allaah (Ta´ala). Mtu kama huyu mfano wake ni kama yule mwenye kuharamisha kile Allaah alichohalalisha. Kama ambavyo Allaah peke Yake ndiye ana haki ya kusema ni kipi cha halali na cha haramu, kadhalika ni Yeye ndiye mwenye haki ya kusema ni nani kafiri na ni nani ambaye si kafiri.

2 – Kuhusiana na la pili, amemsifu muislamu kwa wasifu ulio kinyume. Amesema kuwa ni kafiri pamoja na kuwa mtu huyo ametakasika na hilo. Yeye ndiye ana haki zaidi ya ukafiri huo kumrudilia. Katika “as-Swahiyh” ya Muslim imethibiti ya kwamba ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu akimkufurisha ndugu yake, basi itamrudilia mmoja wao.”[6]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ima itakuwa kama ilivyosema, au itamrudilia yeye.”

Vilevile imepokelewa humo kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kumwita mwenziwe “kafiri” au akasema “adui wa Allaah”, na asiwe hivyo, itamrudilia yeye mwenyewe.”[7]

Bi maana itamrejelea yeye.

Maneno yake katika Hadiyth ya Ibn ´Umar “Ima itakuwa kama ilivyosema” ina maana ya kwamba imeafikiana na hukumu ya Allaah (Ta´ala). Kadhalika maneno yake katika Hadiyth ya Abu Dharr “na asiwe hivyo” bi maana haiafikiani na hukumu ya Allaah.

Hii ndio dhambi ya pili, nayo ni tuhuma za ukafiri zinamrudilia yeye ikiwa ndugu yake ametakasika na hilo. Hii ni dhambi kubwa kabisa na kuna khatari akatumbukiaemo. Mara nyingi huwa hivyo, yule ambaye ana haraka ya kumtuhumu muislamu ukafiri anakuwa ni mwenye kujikweza kwa matendo yake na wakati huohuo anawadharau wengine. Hivyo anakuwa amekusanya kati ya kujiona katika matendo yake, jambo ambalo linaweza kupelekea yakaharibika, na kiburi, jambo ambalo linaweza kupelekea katika adhabu ya Allaah (Ta´ala) Motoni. Imepokelewa katika Hadiyth iliyopokelewa na Ahmad na Abu Daawuud kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Kiburi ni shuka Yangu ya juu na ukuu ni kikoi Changu cha chini. Mwenye kuzozana na Mimi kwa kimoja katika hivyo, basi nitamtupa Motoni.””[8]

Kabla ya kumhukumu mwengine ukafiri inatakiwa kuzingatia mambo mawili.

1 – Dalili kutoka katika Kitabu na Sunnah kuwa kitendo hicho kweli ni kufuru ili asimzulie Allaah uongo.

2 – Kwamba hukumu inaafikiana na mtu huyo kwa njia ya kwamba masharti ya kumhukumu ukafiri yameenea na hakuna vikwazo.

Miongoni mwa masharti muhimu sana ni mtu awe na ujuzi wa uhalifu wenye kuwajibisha ukafiri. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Na atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, basi Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kuishia!” (04:115)

Ili mtu aadhibiwe Motoni, imeshurutishwa apingane na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kubainikiwa na uongofu.

Lakini imeshurutishwa vilevile mtu awe ni mjuzi wa uhalifu wake unapelekea katika nini au inatosheleza mtu awe ni mjuzi wa uhalifu wake ijapokuwa hajui matokeo yake? Jibu ni hilo la pili. Inatosheleza kwa mtu awe ni mjuzi wa uhalifu wake ili ahukumiwe yale hukumu inayopelekea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemuwajibishia yule mwenye kufanya jimaa mchana wa Ramadhaan atoe kafara kwa sababu alijua uhalifu wake pamoja na kuwa hajui kafara yenyewe. Vievile mzinifu ambaye kishawahi kuingia ndani ya ndoa na anajua kuwa ni haramu, atapigwa mawe, ingawa hajui kuzini kwake kutapelekea katika adhabu gani. Angeyajua, huenda asingeyafanya.

Miongoni mwa vizuizi vya kumpachika mtu ukafiri, ni kuwa mtu alazimishwa katika matendo ya makafiri. Amesema (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya imani yake [atapata adhabu] isipokuwa yule ambaye ametenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu.” (16:106)

Kizuizi kingine ni kama fikira na makusudio yake yanaacha kufanya kazi kwa njia ya kwamba hajui anachokisema. Hili linaweza kutokamana na furaha, huzuni, ghadhabu, khofu ya kupindukia na mfano wa hayo. Amesema (Ta´ala):

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini [itakuwa dhambi] katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu – na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (33:05)

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim[9] imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hufurahishwa na tawbah ya mja Wake pale anapotubia Kwake, kuliko jinsi mmoja wenu anavyompata mnyama wake aliyekuwa amepotea katika ardhi ya wazi. Mnyama huo alikuwa na chakula na kinywaji chake. Alipokata tamaa kabisa juu ya mnyama wake, akaenda kulala chini ya kivuli cha mti. Alipokuwa katika hali hiyo, tahamaki akamuona mnyama wake karibu yake na akamshika kamba zake. Halafu akasema kwa furaha kubwa: “Ee Allaah! Wewe ndiye mja Wangu na mimi ndiye Mola Wako”.”

Kizuizi kingine ni mtu awe na hoja tata ambapo anaifasiri na kuielewa kufuru kimakosa kwa njia ya kwamba anafikiria kuwa ni haki. Mtu huyu hakusudii kufuru wala kwenda kinyume. Watu kama hawa wanaingia katika maneno Yake (Ta´ala):

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ

“Na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini [itakuwa dhambi] katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu.” (33:05)

Isitoshe hilo ndio upeo wa uwezo wake. Kwa ajili hiyo anaingia katika maneno Yake (Ta´ala):

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake.” (02:286)

[Ibn Qudaamah] amesema katika “al-Mughniy[10]:

“Vivyo hivyo – yaani ni kafiri – endapo atahalalisha kuwaua watu wasiokuwa na hatia na kuchukua mali zao akafanya hivo bila ya utata wala kuelewa kimakosa. Ikiwa ni kutokana na kuelewa kimakosa, kama Khawaarij, tumetaja ya kwamba wanachuoni wengi wa Fiqh hawaonelei kuwa ni makafiri. Mambo ni namna hii pamoja na kuwa wamehalalisha damu na mali za waislamu kumwagwa. Isitoshe walifanya hayo huku wakijikurubisha kwa Allaah (Ta´ala).”

Halafu akasema:

“Ni jambo lenye kujulikana kuwa mfumo wa Khawaarij wanaonalea kuwa wengi katika Maswahabah na walio baada yao ni makafiri. Walihalalisha damu na mali zao kuchukuliwa na huku wakiitakidi kujikurubisha kwa Mola Wao. Pamoja na haya, wanachuoni wa Fiqh hawakuonelea kuwa ni makafiri kutokana na kuelewa kwao kimakosa. Hali kadhalika inahusiana na kila mwenye kuhalalisha kitu cha haramu kutokana na kuelewa kimakosa.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”[11]:

“Bid´ah ya Khawaarij inatokamana na ufahamu wao mbaya wa Qur-aan. Hawakukusudia kwenda kinyume nayo, lakini walifahamu kimakosa kile kilichofahamishwa nayo. Hivyo wakadhania kwamba inapelekea kumkufurisha kila mtenda dhambi.”

Katika ukurasa wa 210 amesema:

“Khawaarij wameenda kinyume na Sunnah ilihali Qur-aan imetuamrisha kuifuata. Wakawakufurisha waumini ilihali Qur-aan inatuamrisha kuwapenda… Wakaanza kufuata Aayah za Qur-aan zisizokuwa wazi ambapo kwa ujinga wakaifasiri kwa ufahamu wa kimakosa. Hawakuwa na maarifa juu ya tafsiri yake wala ubobeaji katika elimu. Hawakuwa wakifuata Sunnah wala kurejea katika mkusanyiko wa waislamu wanaofahamu Qur-aan.”

Vilevile amesema[12]:

“Maimamu wamekubaliana juu ya kuwakemea Khawaarij na kuonelea kuwa ni wapotevu. Wanachotofautiana tu ni kama, ni makafiri au sio makafiri. Kuna maoni mawili yanayojulikana juu ya masuala haya.”

Lakini amesema kadhalika[13]:

“Hakuna yeyote katika Maswahabah aliyekuwa akiwakufurisha. Si ´Aliy bin Abiy Twaalib wala mwengine yeyote. Walikuwa wakionelea kuwa ni waislamu madhalimu na wakandamizaji. Nimetaja mapokezi mengi kutoka kwao sehemu nyingi.”

Kisha akasema[14]:

“Haya ndio yaliyopokelewa kutoka kwa maimamu kama vile Ahmad na wengine.”

Halafu akasema[15]:

“Khawaarij ni watu wa uasi ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kaamrisha kuwapiga vita. ´Aliy bin Abiy Twaalib ambaye alikuwa ni mmoja katika makhaliyfah waongofu aliwapiga vita. Kadhalika maimamu wa dini kati ya Maswahabah, Taabi´uun na waliokuja baada yao wameafikiana juu ya kuwapiga vita. Hakuna aliyewakufurisha, si ´Aliy bin Abiy Twaalib, Sa´d bin Abiy Waqqaas wala Swahabah mwingine. Ijapokuwa waliwapiga vita, walikuwa wakionelea kuwa ni waislamu. ´Aliy hakuanza kuwapiga vita isipokuwa baada ya kumwaga damu na kushambulia mali ya waislamu. Hapo ndipo alianza kuwapiga vita ili kuzuia dhuluma na manyanyaso yao, sio kwa sababu walikuwa ni makafiri. Kwa ajili hiyo ndio maana hakuwateka wanawake wao. Wala mali zao hakuzifanya kuwa ni mateka. Ikiwa watu hawa ambao umethibiti upotevu wao kwa Maandiko na Maafikiano, hawaonelewi kuwa ni makafiri pamoja na kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha kuwapiga vita, vipi kwa mapote yanayoenda kinyume ambayo haki imewatatiza katika mambo ambayo wajuzi kuliko wao walikosea! Haijuzu kwa yeyote kutoka katika mapote haya kumkufurisha mwingine. Haijuzu kuhalalisha damu wala mali kuchukuliwa, hata kama watakuwa na Bid´ah iliyothibiti. Mtu asemeje ikiwa hao wanaowakufurisha pia ni watu wa Bid´ah? Bali kuna uwezekano Bid´ah za watu hawa zikawa ni mbaya zaidi. Mara nyingi wote huwa ni wajinga juu ya kile wanachotofautiana.”

Kisha akasema:

“Endapo muislamu ni mwenye kuelewa kimakosa vita au kukufurisha, hakufuru.”

Halafu katika ukurasa wa 288 akasema:

“Wanachuoni wametofautiana juu ya masemezo ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); hukumu zake ni zenye kuthibiti kwa waja kabla ya kusimamikiwa na hoja au hapana? Kuna maoni matatu katika madhehebu ya Ahmad na wengine… Sahihi ni yale yanayofahamishwa na Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا

“Na Hatukuwa wenye kuadhibu yeyote mpaka Tupeleke Mitume.” (17:15)

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume hali ya kuwa ni wabashiriajina waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya [kuletwa] Mitume.” (04:165)

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na ya Muslim imepokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna yeyote anayependa udhuru kama Allaah. Kwa ajili hiyo ndio maana amewatuma Mitume hali ya kutoa bishara njema na maonyo.”[16]

Kwa kufupisha ni kwamba mjinga ni mwenye kupewa udhuru kwa maneno na matendo yake ya kufuru. Kadhalika ni mwenye kupewa udhuru kwa maneno na matendo yake ya kimadhambi. Haya yamethibitishwa kwa dalili za Kitabu, Sunnah, utafiti na maneno ya wanachuoni.

[1] Fataawaa wa Masaa-il ash-Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 5-6, katika Majmuu´ Mu’allafaat-ish-Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, mjeledi wa 2.

[2] (01/134).

[3] (08/131).

[4] (03/229).

[5] ad-Durar as-Sunniyyah (1/56).

[6] (111).

[7] (112)

[8] Ahmad (2/376), Abuu Daawuud (4048) na Ibn Maajah (4174).

[9] (2104).

[10] (08/131).

[11] (13/30).

[12] (28/518).

[13] (07/217).

[14] (28/518).

[15] (03/282).

[16] al-Bukhaariy (7416) na Muslim (1499).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Fitqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 23/04/2022