22. Kusoma nyuma ya imamu wakati wa swalah ya kunyamaza

Kuhusu katika swalah za kusoma kwa kunyamaza, aliwakubalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusoma ndani yake. Jaabir alisema:

“Tulikuwa tukisoma Dhuhr na ´Aswr katika zile Rak´ah mbili za mwanzo al-Faatihah na Suurah nyingine na katika zile Rak´ah mbili za mwisho al-Faatihah peke yake.”[1]

Alichokataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kushawishiwa na kisomo cha mtu. Wakati mmoja pindi aliposwali Dhuhr na Maswahabah wake akasema:

“Ni nani katika nyinyi amesoma:

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى

“Limetakasika Jina la Mola wako Aliye juu?”[2]

Mwanaume mmoja akasema: “Mimi [na sikukusudia kwayo isipokuwa kheri].” Ndipo akasema: “Nilijua kuwa kuna ambaye ananishawishi kwayo.”[3]

Katika Hadiyth nyingine imekuja namna walivyokuwa wakisoma kwa sauti nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema:

“Mmenifanya kuichanganya Qur-aan.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mswaliji anamnong´oneza Mola wake. Hivyo basi atazame vile anavyomnong´oneza. Asipaze sauti yeyote juu ya mwengine kwa Qur-aan.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayesoma herufi moja kutoka katika Kitabu cha Allaah ana thawabu moja na thawabu moja inalipwa mara kumi mfano wake. Sisemi kuwa Alif, Laam na Miym ni herufi moja. Lakini Alif ni herufi moja, Laam ni herufi moja na Miym ni herufi moja.”[5]

[1] Ibn Maajah kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (506).

[2] 87:01

[3] Muslim, Abu ´Awaanah na as-Siraaj.

[4] al-Bukhaariy katika ”Juz’-ul-Qiraa’ah khalf al-Imaam”, Ahmad na as-Siraaj kwa mlolongo wa wapokezi mzuri.

Faida:

Miongoni mwa wanachuoni waliokuwa wakionelea kuwa imewekwa katika Shari´ah kusoma nyuma ya imamu katika zile swalah za kunyamaza na si zile za kusoma kwa sauti ni pamoja na Imaam ash-Shaafi´iy katika maoni yake ya zamani na Muhammad ambaye ni mwanafunzi wa Abu Haniyfah kwa mujibu wa upokezi mmoja. Maoni haya yamechaguliwa na Shaykh ´Aliy al-Qaariy na wanachuoni wengine wa madhehebu. Maoni haya ndio vilevile ya Imaam az-Zuhriy, Maalik, Ibn-ul-Mubaarak, Ahmad bin Hanbal na wanachuoni wengine kutoka katika Muhaddithuun na wengineo na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah pia.

[5] at-Tirmidhiy na al-Haakim kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Kadhalika imepokelewa vilevile na al-Aajurriy katika ”Aadaab Hamalat-il-Qur-aan”. Imetajwa katika ”as-Swahiyhah” (569).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 87-88
  • Imechapishwa: 04/02/2017