21. Uwajibu wa kunyamaza, uharamu wa kufasiri

86- Jengine ni kwamba hili sio jambo ambalo mtu anahitajia kulijua kwa sababu hakuna matendo yanayotokana na hakuna dharurah ya kilazima inayopelekea kulitafiti. Ikiwa sio wajibu basi haijuzu pia kutokana na sababu nyingi. Sababu moja wapo ni kwamba ingelikuwa inafaa kufasiri basi inafaa pia kunyamaza. Katika hali hiyo yule mwenye kunyamaza anakuwa ni mwenye kusalimika kwa maafikiano yenye yakini. Sambamba na hilo yule mwenye kufasiri yuko katika khatari kubwa kwa kitu asichokihitajia. Hili kwa dhati yake halifai. Upande mmoja yule mtu asiyefasiri hakusema juu ya Allaah isipokuwa tu haki. Upande mwingine yule mwenye kufasiri kuna khatari akawa amesema juu ya Allaah pasi na haki, amemsifu kwa kitu ambacho hakujisifu nacho Mwenyewe au amemkanushia kitu ambacho amejisifu nacho Mwenyewe. Hili ni jambo la haramu. Kwa hivyo ni lazima kunyamaza na ni haramu kufasiri.

87- Sababu nyingine ni kwamba ikiwa tamko linaweza kufahamika kwa njia nyingi na likathibitshiwa maana moja pekee, huko itakuwa ni kubahatisha na kumsemea Allaah bila ya elimu. Allaah ameharamisha hilo pale aliposema:

وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“… na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[1]

88- Kuanisha au kulenga tafsiri moja pasi na dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah hiyo ina maana kwamba zile tafsiri zengine zote ni zenye kutupiliwa mbali. Ili mtu aweze kufanya hivo kunahitajika elimu juu ya zile njia zote, uhakika au majazi, neno linaweza kutumika kwa njia moja na likafuta tafsiri na maana zengine zote. Haya yanahitajia kuzizunguka zile lugha zote na kuitambua lugha ya kiarabu barabara, jambo ambalo haliwezekani. Mtu asemeje juu ya yule asiyeijua lugha ya kiarabu na anachoweza ni maneno mawili matatu kwa njia ya kufuata kichwa mchunga?

[1] 07:33

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 40-42
  • Imechapishwa: 20/12/2018