´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 21: Ni ipi Njia iliyonyooka na ni zepi sifa zake?

Jibu: Njia iliyonyooka ni elimu yenye manufaa na matendo mema.

Elimu yenye manufaa ni yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya Qur-aan na Sunnah.

Matendo mema ni kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) kwa kuwa na I´tiqaad ambazo ni sahihi, kutekeleza mambo ya faradhi na yaliyopendekezwa na kujiepusha na yaliyokatazwa. Kwa msemo mwingine inahusiana na kutekeleza haki za Allaah na haki za waja Wake.

Hakuna chenye kutimia katika hayo isipokuwa kwa kumtakasia nia Allaah na kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dini imejengwa juu ya misingi hii miwili. Asiyeitakasa nia yake anatumbukia katika shirki na asiyemfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatumbukia katika Bid´ah.

MAELEZO

Njia iliyonyooka ni njia ya wazi aliyotuachia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama alivyomsifia nayo Mola Wake. Allaah (Subhaanah) ametuamrisha kufuata njia iliyonyooka na akasema.

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!”[1]

Njia nyenginezo ni zile njia za kishaytwaan. Kila njia ina shaytwaan ambaye analingania kwayo. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichora msitari ulionyooka ambapo akasema: “Hii ni njia ya Allaah.” Kisha akachora njia nyenginezo pambizoni na ile njia ilionyooka ambapo akasema: “Hizi ni njia nyenginezo. Katika kila njia yuko shaytwaan ambaye analingania kwayo.” Kisha akasoma:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!”[2]

Abu Shurayh al-Khuzaa´iy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijitokeza kwetu na akasema: “Pateni bishara! Nyinyi hamshuhudii ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah?” Tukasema: “Ndio.” Akasema: “Hakika hii Qur-aan ni kamba; ncha yake moja iko mikononi mwa Allaah na ncha yake nyingine iko mikononi mwenu. Shikamaneni nayo; hakika hamtopotea na wala hamtoangamia baada yake kamwe.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amepiga mfano wa njia iliyonyooka kwa kuchora msitari wenye kunyooka. Njia iliyonyooka ni kule kutekeleza yale yaliyokuja na Qur-aan na Sunnah upande wa I´tiqaad, matendo na ´ibaadah. Njia hiyo iko na matendo, maneno na kujitolea mali kwa ajili ya kutafuta radhi za Allaah (´Azza wa Jall), kama mfano wa kutoa zakaah na kupambana katika njia ya Allaah kwa nafsi na kwa mali, pamoja na kujiepusha na yale maneno na vitendo vyote alivyokataza Allaah. Yule mwenye kuyatekeleza haya basi kwa hakika anakwenda sambamba na njia ilionyooka.

Lakini hata hivyo matendo yanahitaji elimu ambayo mtu atajenga juu yake. Ambaye atafanya matendo na akajitahidi kufanya ´ibaadah pasi na elimu atatumbukia katika upotevu. Hayo ndiyo yanafanywa na Khawaarij, Suufiyyah, Shiy´ah na wengineo. Ni lazima kwa kila mmoja kwenda mbio kwelikweli kujifunza elimu yenye manufaa. Elimu hiyo inatakiwa iwe inatokana na Qur-aan na Sunnah chini ya wanachuoni katika Ahl-ul-Hadiyth wanaofuata mfumo wa Salaf, kwa msemo mwingine mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Yeyote mwenye kumwabudu Allaah pasi na elimu basi atamtumbukia kwenye upotevu. Upotevu huo unaweza kuwa na maana ya kuzidisha na kuchupa mpaka, au wakati mwingine kuzembea. Mja hasalimiki na upetukaji na uzembeaji isipokuwa kwa elimu yenye manufaa. Kwa ajili hiyo ndio maana Shaykh (Rahimahu Allaah) amefasiri njia iliyonyooka kwamba ni elimu yenye manufaa na matendo mema. Amesema:

Elimu yenye manufaa ni yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya Qur-aan na Sunnah.

Matendo mema ni kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) kwa kuwa na I´tiqaad ambazo ni sahihi, kutekeleza mambo ya faradhi na yaliyopendekezwa na kujiepusha na yaliyokatazwa.”

Maneno haya ni yenye kuenea na yanastahiki kuandikwa kwa maji ya dhahabu. Yote haya yanarejea katika kumtakasia nia Allaah na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kisha akasema:

Hakuna chenye kutimia katika hayo isipokuwa kwa kumtakasia nia Allaah na kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dini imejengwa juu ya misingi hii miwili. Asiyeitakasa nia yake anatumbukia katika shirki na asiyemfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatumbukia katika Bid´ah.”

Huu ni mfano mzuri wenye upeo wa hali ya juu. Elimu yenye manufaa ni kama mfano wa njia na matendo mema ni kama mfano wa kutembea juu ya njia hiyo. Yule  asiyeijua njia hupotea na hutumbukia katika mambo yenye kumdhuru. Yule mwenye kuijua njia na asipite juu yake basi huenda kimakosa. Njia iliyonyooka ni ile ilio wazi ambayo haina kupindapinda. Ee Allaah! Tunakuomba utuwafikisha katika elimu yenye manufaa na mtendo mema!

Njia hapa duniani ni kitu cha kimaana na inahusiana na kuyafuata yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah amesema:

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu.”[4]

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

“Wale walioamini na hawakuchanganya imani zao na dhuluma, hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.”[5]

Siku ya Qiyaamah njia itakuwa yenye kuhisiwa. Njia itawekwa juu ya Moto; ni yenye makali zaidi kuliko upanga, nyembamba zaidi kuliko unywele. Hakuna atayeokoka kupita juu yake isipokuwa yule ambaye alitendea kazi Qur-aan na Sunnah. Kumepokelewa juu ya hilo Hadiyth nyingi namna ambavo waja watapita juu ya njia. Baadhi watapita kama kupepesa kwa macho, wengine watapita kama mweko, wengine watapita kama upepo, wengine watapita kama farasi waendao mbio, wengine kama ngamia. Wako ambao watapita wakikimbia, wengine watapita wakitambaa, wengine watapita kwa kutembea na wengine wakitambaa kwa matumbo yao. Yule ambaye ameachwa nyuma kwa matendo yake hatoharakishwa kwa nasaba yake. Kadri ambavo mtu atakuwa ameshikamana barabara na haki, basi ndivo atapita kwa haraka zaidi juu ya njia siku ya Qiyaamah. Allaah hamdhulumu yeyote katika waja Wake.

[1] 6:153

[2] an-Nasaa’iy (6/343), Ahmad (1/435), ad-Daarimiy (202) na al-Bazzaar (57113).

[3]Ibn Hibbaan (122). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (713).

[4] 07:03

[5] 06:82

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 109-113
  • Imechapishwa: 28/10/2021