21. Mlango kuhusu kuchupa mipaka katika makaburi ya watu wema hupelekea huyafanya kama masanamu yaabudiwayo badala ya Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Maalik amepokea katika “al-Muwattwa´” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Nakuomba usilifanye kaburi langu kuwa sanamu lenye kuabudiwa. Ghadhabu za Allaah huwa kali kwa watu ambao wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”[1]

Ibn Jariyr amepokea kwa cheni ya wapokezi wake kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Mujaahid ambaye amesema kuhusiana na maneno ya Allaah:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنثَىٰ

”Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat, mwengine wa tatu [mliokuwa mkiwaabudu]? Je, nyinyi mna wana wa kiume Naye ana wana wa kike?” (an-Najm 53:19-21)

“al-Laat alikuwa akiwapikia uji [mahujaji]. Alipokufa ndipo watu wakawa wakikusanyika kwa muda mrefu kwenye kaburi lake.”

Namna hii ndivyo alivyosema Abul-Jawzaa´ kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Alikuwa akitengeneza uji kwa ajili ya mahujaji.”

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi, wenye kuyafanya ni mahali pa kuswalia na wanaoyatilia mataa.”[2]

Wameipokea watunzi wa Sunan.

MAELEZO

Haya ni kweli kama ilivyotangulia. Kuchupa mipaka kunamfanya yule mwenye kufanyiwa upetukaji kuwa ni mwabudiwa badala ya Allaah. Kwa ajili hii wakati baadhi ya watu walipoanza kuchupa mipaka kwa baadhi ya watu wema wakawaabudu badala ya Allaah. Kama mfano wa makaburi ya waja wema kama mfano wa kaburi la al-Hasan, al-Husayn na la Faatwimah. Kadhalika Ummah huu umechupa mipaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na matokeo yake wakamuabudu, wakamuomba uokozi na kumuomba badala ya Allaah. Pindi watu wa Nuuh walipopetuka mipaka kwa watu wema wakawaabudu, kama ilivyokwishatangulia.

1- Maalik amepokea katika “al-Muwattwa´” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Nakuomba usilifanye kaburi langu kuwa sanamu lenye kuabudiwa. Ghadhabu za Allaah huwa kali kwa watu ambao wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Upokezi huu umepokelewa vilevile na ´Atwaa´ bin Yasaar na Zayd bin Aslam bila ya Swahabah katika cheni ya wapokezi kama vile Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ghadhabu za Allaah huwa kali… “

Kwa sababu wanapojenga misikiti juu yake wanakuwa wamefanya ni waungu wanaoabudiwa badala ya Allaah. Wanaanza kuwaadhimisha, kuyazunguka, kuwaomba msaada na kuyawekea nadhiri. Pindi watu wa at-Twaaif walipochupa mipaka kwa al-Laat wakawa ni wenye kumuabudu badala ya Allaah. Huu ni mwenendo wa wakale na wa waliokuja nyuma. Kuyajengea makaburi na kuyaadhimisha kunayafanya kuwa ni waungu wanaoabudiwa badala ya Allaah. Njia inapelekea katika lengo.

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi, wenye kuyafanya ni mahali pa kuswalia na wanaoyatilia mataa.”

Hadiyth inafahamisha juu ya kwamba ni haramu kwa wanawake kuyatembelea makaburi. Haya ndio maoni sahihi kwa mujibu wa dalili. Kadhalika Hadiyth imepokelewa na Hassaan bin Thaabit na Abu Hurayrah. Kuyatembelea makaburi ni jambo linalowahusu wanaume tu.

Kama tulivyotangulia kusema kwamba kuyafanya makaburi ni mahali pa kuswali ni kujifananisha na mayahudi na manaswara na vilevile ni njia miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki.

Haijuzu kwa wanawake kuyatembelea makaburi hata kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile. Haya ndio maoni sahihi kwa sababu Hadiyth ni zenye kuenea. Imepokelewa vilevile kwa tamko “wanawake wenye kuyatembelea makaburi sana”.

Inajuzu kuapa kwa Qur-aan kwa sababu ni maneno ya Allaah.

[1] Maalik (414), ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (1587) na Ibn Abiy Shaybah (7544). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (750).

[2] Abu Daawuud (3236), at-Tirmidhiy (320), an-Nasaa’iy (2043) na Ahmad (2030). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (225).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 05/10/2018