Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ni jambo la muhali katika akili na dini ikawa taa lenye kuangaza ambalo Allaah kwalo amewatoa watu kutoka vizani na kuwaingiza kwenye nuru, akateremsha Kitabu kwa haki ili kuhukumu baina ya watu katika yale waliyotofautiana, kumteua kuwa marejeo juu ya ile mizozo ya kidini, akalingania kwa Allaah na kwenda katika njia Yake kwa dini Yake juu ya elimu na Allaah ameeleza kwamba amemkamilishia yeye na Ummah wake dini na neema yao – ni jambo muhali kabisa kutokana na hili na mengine kwamba ameacha mlango unaozungumzia kumwamini Allaah na kumtambua ukawa ni wenye kubabaisha na wenye kutatiza. Haiwezekana kwamba aliacha kubainisha majina na sifa ambazo zinamuwajibikia Allaah, zinazofaa na ambazo hazifai.

MAELEZO

Haiwezekani kabisa kwamba Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye hizi ndio sifa zake, awe hakuwabainishia na kuwawekea watu wazi majina na sifa za Allaah na baadaye eti zikaja takataka kama vile Jahmiyyah, Mu´tazilah na vifaranga vyao na kudai kuwa maandiko haya yanayozungumzia sifa si ya hakika na kwamba udhahiri wake ni upotofu, na hivyo haitakiwi kuyaamini. Nadharia hiyo maana yake ni kumtuhumu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kakosea, kupotosha au alificha, kwa sababu hakubainisha kuwa hayatakiwi kufahamika kwa udhahiri wake. Kwa maana nyingine ima Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakujua maana ya maandiko haya, jambo ambalo ni kumtuhumu ujinga, au aliyajua lakini akaamua kutoyabainisha, jambo ambalo ni kumtuhumu kuificha haki. Hakuna chochote katika hayo kinachowezekana juu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mambo yangelikuwa hivo basi asingelikuwa ni siraji yenye kuangaza anayewatoa watu kutoka katika viza na kuwaingiza ndani ya nuru. Bali nadharia hiyo maana yake ni kwamba amekuja ili kuwazidishia kuzama ndani ya upotofu. Kwa maana nyingine ni kwamba haiwezekani Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyetumwa ili kuwaongoza watu akairuka mada hii kuhusu majina na sifa za Allaah. Kwa ajili hiyo asiwabainishie watu kuwa maandiko haya yanatakiwa kufahamika kama ulivyo udhahiri wake au ni mafumbo tu? Anayefanya hivo ima akawa ni mjinga au mwenye kuficha elimu. Allaah amemtakasa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na mambo yote hayo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 48
  • Imechapishwa: 29/07/2024