117- Kisha mtu arudi Minaa na abaki huko yale masiku ya Tashriyq pamoja na nyusiku zake.

118- Kila siku baada ya jua kupinduka atarusha mawe katika zile nguzo tatu. Katika kila nguzo kutarushwa vijiwe vidogo saba, kama ilivyotangulia kuelezwa (86-90).

119- Mtu anatakiwa kuanza na ile nguzo ya kwanza ilio karibu na msikiti wa Khayf. Mtu atapomaliza kuitupia mawe, basi atasogea mbele kidogo upande wake wa kulia. Huko atasimama hali ya kuelekea Qiblah na atasimama kwa kipindi kirefu na kuomba na huku ameinyanyua mikono yake[1].

120- Kisha ataiendea nguzo ya pili na airushie mawe vilevile.  Halafu ataenda upande wa kushoto. Hapo atasimama hali ya kuelekea Qiblah na atasimama kwa kipindi kirefu na kuomba na huku ameinyanyua mikono yake[2].

121- Kisha ataiendea nguzo ya kurusha mawe ya tatu, nayo ndio nguzo ya ´Aqabah, na airushie mawe. Hapa Ka´bah itakuwa upande wake wa kushoto na Minaa upande wake wa kulia. Lakini hatosimama hapo[3].

122- Katika siku ya pili na siku ya tatu atarusha mawe vivyo hivyo.

123- Inafaa kwake kuondoka baada ya kurusha mawe katika siku ya pili bila ya kulala hapo kwa ajili ya kurusha mawe katika siku ya tatu. Hilo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ ۚفَمَن تَعَجَّلَ فِي يَوْمَيْنِ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ وَمَن تَأَخَّرَ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚلِمَنِ اتَّقَىٰ

“Mdhukuruni Allaah katika zile siku zinazohesabika. Atakayeharakisha kuondoka katika siku mbili, basi si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa yule mwenye kuogopa.”[4]

Lakini hata hivyo kubaki hapo kwa kuchelewa kwa ajili ya kurusha mawe ndio bora zaidi, kwa sababu ni Sunnah[5].

124- Sunnah ni kufanya mitindo ya ´ibaadah iliotangulia kwa mpangilio:

 1. Kurusha mawe.
 2. Kuchinja.
 3. Kunyoa.
 4. Twawaaf-ul-Ifaadhwah.
 5. Sa´y kwa ambaye ni Mutamatti´.

Lakini endapo mtu atatanguliza limoja kabla ya lingine hakuna neno. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hapana vibaya. Hapana vibaya.”

125- Mambo yafuatayo yanajuzu kwa yule ambaye ni mwenye udhuru kutokamana na kurusha mawe.

 1. Kuacha kulala Minaa. Ibn ´Umar amesema:

“al-´Abbaas alimwomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ruhusa ya kulala Makkah katika nyusiku za Minaa kwa ajili ya kunywesheleza ambapo akampa idhini.”[6]

 1. Kurusha mawe siku moja kwa ajili ya siku mbili. ´Aaswim bin ´Adiyy amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapa idhini wachunga ngamia ya kuacha kulala ili waweze kurusha mawe siku ya Nahr. Kisha wakusanye urushaji wa vijiwe vya siku mbili baada ya siku ya Nahr na warushe katika siku moja wapo.”[7]

 1. Vilevile walipata ruhusa ya kurusha usiku. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mchungaji anarusha usiku na anachunga [wanyama] mchana.”[8]

126- Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwake kuitembelea Ka´bah na kuitufu kila usiku katika nyusiku za Minaa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya hivo[9].

127- Ni wajibu kwa mahujaji kuhifadhi vipindi vitano vya swalah pamoja na mkusanyiko katika yale masiku ya Minaa. Ikiwa ni wepesi kwake basi bora ni yeye aziswali katika msikiti wa Khayf. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mitume sabini waliswali katika msikiti wa Khayf.”[10]

128- Akimaliza kurusha mawe katika siku ya pili, au ya tatu, katika masiku ya Tashriyq basi atakuwa amemaliza utaratibu wa ´ibaadah za hajj. Kisha aende Makkah na abaki huko vile Allaah atakuwa amemwandikia. Apupie kutekeleza swalah pamoja na mkusanyiko, khaswa khaswa katika msikiti Mtakatifu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah moja katika msikiti wangu ni bora mara elfu moja kuliko katika misikiti mingine isipokuwa tu msikiti Mtakatifu. Swalah moja katika msikiti Mtakatifu ni bora mara laki moja kuliko katika misikiti mingine.”[11]

129- Akithirishe kutufu na kuswali katika wakati wowote ataotaka. Ni mamoja atafanya hivo usiku au mchana. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na nguzo mbili, nyeusi na ya kiyemeni:

“Mtu atapozigusa atafutiwa madhambi yake. Yule atakayetufu Nyumba basi hatonyanyua mguu wala hatoweka mguu chini isipokuwa Allaah atamwandikia jema moja, atamfutia dhambi na atampandisha daraja moja. Yule atakayeenda mizunguko saba, atalipwa kama ambaye ameacha mtumwa huru.”[12]

Vilevile amesema:

“Enyi wana wa ´Abd Manaaf! Msimzuie yeyote kutufu Nyumba hii wala kuswali katika wakati wowote ataotaka. Ni mamoja usiku au mchana.”[13]

[1] Yote haya yamethibiti katika Hadiyth ya Ibn Mas´uud kwa al-Bukhaariy na Muslim na wengineo. Yale yaliyoko katika baadhi ya vitabu vya utaratibu wa hajj kwamba mtu anatakiwa kuelekea Qiblah wakati wa kurusha mawe katika nguzo ya ´Aqabah, ni jambo linalokwenda kinyume na Hadiyth hii Swahiyh. Si kwamba ni jambo linalokwenda kinyume pekee, bali ni munkari. Hayo nimeyabainisha katika ”adh-Dhwa´iyfah” (4864).

[2] Tazama marejeo yaliyotangulia.

[3] Tazama marejeo yaliyotangulia.

[4] 02:203

[5] Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Ikitokea jua likazama naye bado akingali Minaa, basi abaki papohapo ili aweze kurusha mawe pamoja na watu wengine katika ile siku ya tatu.”

Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi tofauti na vile alivyoonelea Ibn Hazm katika “al-Muhallaa” (7/185). an-Nawawiy amestadili maoni yao kwa kile kinachopata kufahamika katika maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن تَعَجَّلَ فِي يَوْمَيْنِ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ

“Atakayeharakisha kuondoka katika siku mbili, basi si dhambi juu yake.”

Amesema katika “al-Majmuu´” (8/283):

“SIku inahusiana na mchana pasi na usiku.”

Vilevile kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwa ´Umar na mwanawe ´Abdullaah ambaye amesema:

“Yule ambaye jioni itamkuta pale katika siku ya pili Minaa, basi abaki pale mpaka siku ya pili asubuhi mpaka aweze kuondoka pamoja na wengine.”

Matamshi ya Ibn ´Umar katika “al-Muwattwaa´” yako kama ifuatavyo:

“Mtu asiondoke mpaka ataporusha mawe kwenye nguzo ya kurusha mawe siku ya pili yake.”

Imaam Muhammad ameipokea kutoka kwa Maalik katika ”al-Muwattwaa’” yake (233) na akasema:

“Haya ndio maoni yetu, maoni ya Abu Haniyfah na ya wengi katika wanachuoni.”

[6] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (1079).

[7] Wameipokea watunzi wa Sunan. Kundi la wanachuoni wameonelea kuwa ni Swahiyh. Imetajwa katika marejeo yaliyotangulia (1080).

[8] Hadiyth ni nzuri. Ameipokea al-Bazzaar, al-Bayhaqiy na wengineo kutoka kwa Ibn ´Abbaas. Haafidhw amesema kuwa cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Kadhalika ina njia zengine kama ushahidi ambazo nimezitaja katika ”as-Swahiyhah” (2477).

[9] Ameipokea al-Bukhaariy ikiwa na cheni ya wapokezi iliopungua (Mukhtaswar al-Bukhaariy (287) ilihali wako wengine ambao wameipokea ikiwa na cheni ya wapokezi ilioungana. Nimewataja katika ”as-Swahiyhah” (804)).

[10] Ameipokea at-Twabaraaniy na adh-Dhwiyaa’ al-Maqdisiy katika ”al-Mukhtaarah”. al-Mundhiriy amesema kuwa cheni ya wapokezi wake ni nzuri, mambo ni kama alivosema kwa kuzingatia ina njia zengine zinazoitolea ushahidi. Hilo nimelihakiki katika ”Tahdhiyr-us-Saajid min Ittikhaad-il-Qubuur Masaajid” (uk. 106-107).

[11] Ameipokea Ahmad na wengineo kutoka kwa Jaabir. Cheni ya wapokezi wake ni nzuri na imesahihishwa na kundi la wanachuoni ambao nimewataja katika  ”al-Irwaa’” (1129).

[12] Ameipokea at-Tirmidhiy na wengineo. Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaa, al-Haakim na wengineo wameonelea kuwa ni Swahiyh. Imetajwa katika ”al-Mishkaat” (258) na ”at-Targhiyb” (2/120-122).

[13] Wameipokea watunzi wa Sunan na wengineo. at-Tirmidhiy, al-Haakim na adh-Dhahabiy wameisahihisha. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (481).

 • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
 • Mfasiri: Firqatunnajia.com
 • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 37-40
 • Imechapishwa: 20/07/2018