Swali: Wakati wa likizo katika Ramadhaan baadhi wanakesha mpaka Fajr kisha wanalala mpaka wakati wa adhaana ya Maghrib. Ni ipi hukumu ya tabia hii?

Jibu: Kukesha nyusiku za Ramadhaan ima kukatokana na ´ibaadah au matendo yaliyoruhusiwa au matendo yaliyoharamishwa. Ikiwa kunatokana na ´ibaadah basi jambo hilo ni zuri na limependekezwa. Kwa sababu imependekezwa kuzihuisha nyusiku za Ramadhaan kwa Dhikr, du´aa, kusoma Qur-aan, swalah na mfano wake, na khaswakhaswa zile nyusiku kumi za mwisho. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akizitumia zile nyusiku ishirini za mwanzo katika kuswali na kulala. Kunapoingia lile kumi la mwisho, basi anafunga vizuri kikoi chake na kujiepusha.”[1]

Ama ikiwa kukesha nyusiku ni katika mambo yaliyoruhusiwa, basi kitendo hicho kimechukizwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anachukizwa na kulala kabla ya ´Ishaa na kuzungumza baada yake. Ikiwa kukesha kunatokana na kitu cha haramu, pasi na kujali ni kitu gani, basi hapana shaka kuwa ni haramu. Aina zote za kukesha ikiwa zinapelekea kukosa jambo la wajibu basi ni haramu. Kama ambaye inampita swalah kwa sababu amekesha usiku na kulala mchana. Ni haramu. Bali kunakhofiwa yule mwenye kufanya hivo na ndio mazowea yake akawa miongoni mwa wale wenye kuacha swalah kwa kuzembea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi yule atakayeiacha amekufuru.”[2]

Yapo maandiko mengine yanayojulisha juu ya utukufu wa jambo la swalah na ukhatari uliopo juu ya dini ya muislamu kwa yule mwenye kuiacha. Kwa hiyo ni lazima kwetu sote kupupia na kujitilia umuhimu sisi wenyewe na wale ambao wako chini ya usimamizi wetu. Allaah atuwafikishe sote katika yale anayoyapenda na kuyaridhia.

[1] Ahmad (25136).

[2] at-Tirmidhiy (2621), an-Nasaa’iy (463) na Ibn Maajah (1079). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 06/04/2022