Swali: Mara nyingi mwanamke wa Kiislamu anatumia muda wake mwingi jikoni akipika aina mbalimbali ya vyakula, jambo ambalo linamfanya kukosa sehemu kubwa ya wakati wa Ramadhaan. Ni kipi unachomnasihi?

Jibu: Allaah ameutaja mwezi wa Ramadhaan uliyobarikiwa na kwamba ni msimu mtukufu maeneo mengine katika Kitabu Chake. Amesema (Ta´ala):

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ

“Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa ndani yake Qur-aan ili iwe ni mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na upambanuo wa haki na batili.”[1]

al-Bukhaariy amepokea kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Unapoingia mwezi wa Ramadhaan hufunguliwa milango ya mbingu, hufungwa milango ya Moto na mashaytwaan wakafungwa minyororo.”[2]

Imekuja kwa Muslim:

“… hufunguliwa milango ya rehema.”

at-Tirmidhiy ameongeza:

“Unapoingia mwezi wa Ramadhaan hufunguliwa milango ya mbingu, hufungwa milango ya Moto na mashaytwaan wakafungwa minyororo. Huita mwitaji: “Ee mwenye kutaka kheri! Sogea! Ee mwenye kutaka shari! Koma!” Allaah ana waachwa huru na Moto na hayo yanakuwa kila usiku.”[3]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia. Yule atakayesimama usiku wenye Cheo kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.”[4]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.”[5]

Zipo dalili nyingi zinazobainisha ubora wa mwezi wa Ramadhaan na kwamba ni wakati wenye ubora ambapo thawabu zinalipwa maradufu na kufutiwa madhambi. Kwa hiyo muislamu wa kiume na muislamu wa kike wanatakiwa kutumia mwezi huu vizuri na wasipoteze wakati katika mambo yasiyokuwa na faida kwao katika maneno ya kipuuzi na mengineyo ambayo ima yanaweza kuahirishwa au kuachana nayo kabisa.

Kuhusu kazi za mwanamke jikoni kitendo hicho ni chema ikiwa anafanya hivo ili kujiandalia kile chakula ambacho yeye na familia yake wanakihitajia. Aidha analipwa thawabu akitarajia malipo kutoka kwa Allaah. Licha ya hivo anaweza kumwabudu Allaah kwa kumtaja, du´aa na kusoma Qur-aan wakati anapika. Hata hivyo ni muhimu kuzindua kuwa wapo baadhi ya dada zetu wa Kiislamu ambao wanapoteza sehemu kubwa ya wakati wao katika kuandaa vyakula zaidi na kuandaa aina mbalimbali ya vyakula ambavyo vinachukua muda mrefu na asivyovihitajia. Bali kuna uwezekano kabisa wa kutosheka na kiasi kidogo. Ala ala pupieni kutumia fursa ya mwezi huu.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (1899) na Muslim (1079).

[3] at-Tirmidhiy (682) n Ibn Maajah (1642).

[4] al-Bukhaariy (1901) na (2014) na Muslim (760).

[5] al-Bukhaariy (37) na Muslim (759).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 06/04/2022