192. ´Aqiydah ilio kati na kati ni ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah

´Aqiydah ya kati na kati ni ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Wanasema kuwa matendo ya waja ni matendo yao kwa njia ya kwamba wamefanya wenyewe kwa kutaka na kupenda kwao, na wakati huohuo Allaah (´Azza wa Jall) ndiye kayaumba:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnavovifanya.”[1]

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

”Allaah ni Muumbaji wa kila jambo, Naye juu ya kila jambo ni mdhamini.”[2]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ

“Enyi watu! Kumbukeni neema za Allaah juu yenu. Je, kuna muumbaji mwingine badala ya Allaah anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi?”[3]

Allaah amepwekeka katika kuumba na kukadiria, na sambamba na hilo mja anao utashi, matakwa na kitendo. Mwenyewe kwa kutaka kwake ndiye anaenda msikitini na ukumbi wa michezo. Kwa sababu yuko na uwezo. Mtu ambaye hana uwezo na nguvu amepewa udhuru na Allaah. Mfano wa watu hao ni wendawazimu na ambaye amelazimishwa; hawafanyi matendo yao kwa kutaka kwao na kwa kukusudia. Yule ambaye yuko na matakwa na makusudio ndiye ambaye anajichagulia kile anachokifanya. Baada ya hapo ima ataadhibiwa au kulipwa thawabu kwa yale aliyoyafanya yeye, na si yale aliyoyafanya Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا يَحْزَنُونَ

“Hakika wale walioamini… ”[4]

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا

”Hakika wale waliokufuru… “[5]

Ameegemeza imani na ukafiri vyote viwili kwao.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[6]

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ

“Atakayemtii Mtume… “[7]

Ameyansibisha matendo kwa waja. Dalili inayoonyesha kuwa mja anao matakwa na makusudio ni maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا

“Hamtotaka chochote isipokuwa atake Allaah; hakika Allaah daima ni Mjuzi, Mwenye hekima.”[8]

Allaah (Subhaanah) amejibitishia kuwa na matakwa na mja kuwa na matakwa, lakini amefanya matakwa ya mja yanakuwa chini ya matakwa Yake (Subhaanah).

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ

“… kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke.”[9]

Bi maana kwa kutaka kwake. Aayah inawaraddi Jabriyyah, ilihali Aayah inayofuata inawaraddi Qadariyyah:

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا

“Hamtotaka chochote isipokuwa atake Allaah; hakika Allaah daima ni Mjuzi, Mwenye hekima.”[10]

[1] 37:96

[2] 39:62

[3] 35:3

[4] 2:62

[5] 02:116

[6] 4:59

[7] 23:52

[8] 76:30

[9] 81:28

[10] 76:30

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 210-212
  • Imechapishwa: 09/04/2025