19. Ubainifu juu ya matamshi ya Qur-aan

Ni kwa nini Salaf walisema kwamba yule mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa ni mtu wa Bid´ah? Bali wako ambao wamefikia kumkufurisha mtu kama huyo.

Walisema hivo kwa sababu tamko hili linaweza kuwa na maana nyingi. Linaweza kutumiwa juu ya tamko lenyewe kama mbavo linaweza kutumiwa juu ya kile kinachotamkwa, ambacho ni Qur-aan. Kutokana na sababu hii ndio maana wakasema kwamba yule mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa ni mzushi.

Baadhi ya wengine wakapambanua suala hili na wakasema sauti ambayo mtu anasoma kwayo Qur-aan, ulimi unaoisoma, koo inayotoa sauti, wino ambao mtu anaandikia kwayo Qur-aan, kalamu ambayo mtu anaandika kwayo, mkono unaoshika kalamu na kuandika na makaratasi ambayo Qur-aan hiyo inaandikwa juu yake – vyote hivi vimeumbwa. Lakini Qur-aan yenyewe ni maneno ya Allaah na haikuumbwa. Matokeo ya vitu hivi vilivyoumbwa ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall). Ama vitu hivi ambavyo mtu anafanyanayo vimeumbwa. Kwa ajili hiyo Shaykh Haafidhw al-Hakamiy (Rahimahu Allaah) amesema:

Sauti ni ya sauti ya msomaji

lakini kile kinachosomwa ni maneno ya Muumba[1]

Mtu wa kwanza ambaye aliandika juu ya maudhui haya ni Imaam al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah). Aliandika kitabu kinachoitwa ”Khalqu Af´aal-il-´Ibaad”. Yafahamu haya ipasavyo na wala usije kutatizwa na mambo!

Dalili juu ya hilo ni ile Hadiyth ambapo siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita pembezoni mwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipokuwa anaswali na kusoma Qur-aan. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakika huyu amepewa sauti nzuri ya Daawuud.”[2]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Lau ningelijua kuwa unanisikiliza basi ningekupambia sauti.”[3]

Sauti na uandishi wa watu unatofautiana. Ni dalili inayoonyesha kuwa sauti inayosoma Qur-aan imeumbwa na Qur-aan yenyewe haikuumbwa.

Imaam Ahmad bin Hanbal alimkemea al-Husayn bin ´Aliy al-Karaabisiy wakati aliposema kuwa matamshi yake ya Qur-aan yameumbwa. Malengo ya makaripio yake ni kwa sababu tamko hilo linaweza kufahamika kwa njia nyingi. Lau angelinyamaza na asikemee basi wazushi wangelitumia kama fursa. Kwa ajili hiyo ndio maana Imaam Ahmad akasitisha hilo.

Pindi tunapoyataja haya ni kwa sababu ya kujifunza. Vinginevyo haifai kwa yeyote kusema kwamba matamshi yake ya Qur-aan yameumbwa. Mwenye kufanya hivo ni mtu wa Bid´ah na ni wajibu kwake kutubu kwa Allaah (´Azza wa Jall).

[1] Tazama ”Ma´aarij-ul-Qabuul” (1/289).

[2] al-Bukhaariy (5048) na Muslim (793).

[3] an-Nasaa’iy (8004) na al-Haakim (5966).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 101-103
  • Imechapishwa: 09/04/2019