Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

139 – Kaburi ima ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi au ni shimo miongoni mwa mashimo ya Moto.

MAELEZO

Pengine mtu akauliza ni vipi maiti ambaye ameshakuwa udongo akaadhibiwa. Allaah ni muweza wa kumuadhibu ingawa ameshakuwa udongo na ni muweza wa kumfanya udongo ukamchoma.

Pengine mtu mwingine akasema kuwa si kila mtu anazikwa, kwa sababu wako ambao wanatupwa baharini na wengine wanaliwa na wanyama wa mwituni. Wataadhibiwa vipi? Ndio, adhabu inamfikia popote anapokuwa. Sivyo tu; hujiliwa na Malaika wawili kumuhoji maswali. Kuyaamini haya ndio kuamini mambo yaliyofichikana na kuamini aliyoeleza Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu ambaye hayaamini hayo na anategemea akili na fikira yake si jengine isipokuwa ni upotofu wa wazi. Adhabu pamoja na neema za ndani ya kaburi ni jambo limefahamishwa na Qur-aan na Sunnah. Bali wanazuoni wanasema kuwa Hadiyth zimepokelewa kwa wingi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) –na ambaye anakadhibisha jambo ambalo limepokelewa kwa mapokezi tele anakuwa kafiri.

Mu´tazilah hawaamini yale matukio yanayotokea ndani ya kaburi kwa sababu ni watu wanaotegemea akili. Wanayajenga mambo juu ya akili zao. Wanaona kuwa dalili za Shari´ah ni za kidhana ilihali dalili za kiakili ni za kihakika. Hiki ndio kipimo chao. Hawa ndio watumiaji akili. Wao na wengineo hii leo wanaotumia akili wanaowaigiliza ndio Mu´tazilah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 195-196
  • Imechapishwa: 10/12/2024