18. Jichagulie sehemu yako ya furaha na huzuni

Miongoni mwa mambo yenye kuwaliwaza waliopewa msiba ni kwamba yule msibiwaji asubiri na atarajie thawabu na amtegemee Allaah huku akitarajia kuwa Allaah atampa kingine kwa kile alichokipoteza, Allaah (Ta´ala) hatomwacha bure tu. Bali atamtunuku kingine badala. Kwa sababu kila kitu isipokuwa Allaah kinaweza kurudishwa mbadala.

Anatakiwa kutambua kuwa sehemu ya msiba wake inatokamana na msimamo wake kwa Allaah. Mwenye kuridhia basi atapata radhi na mwenye kukasirika atapata hasira. Chaguo ni ipi kati ya mambo mawili haya unachokitaka.

Ukionyesha hasira na kutokuwa na shukurani basi wewe ni katika wakhasirikaji.

Ukionyesha huzuni na kughafilika na mambo ya wajibu na makatazo basi wewe ni katika waghafilikaji.

Ukionyesha malalamiko na upungufu wa kutokuwa na subira basi wewe ni katika wakhasirikaji.

Ukionyesha kupingana Naye na kutukana hekima Yake na kubishana na Qadar, basi unagonga mlango wa makadirio yatayokufungukia ili uyapitie. Tahadhari ili adhabu ya Allaah isije kukuangukia. Hakika Yeye ni mjuzi kikamilifu ni nani anayepingana Naye.

Ukionyesha subira na uthabiti kwa ajili ya Allaah basi wewe ni katika wenye kusubiri.

Ukionyesha kuridhika na Allaah na kufurahia maamuzi Yake basi wewe ni katika wenye kufurahi.

Ukionyesha himdi na shukurani basi wewe ni katika wenye kushukuru na wenye kuhimidi.

Ukimuonyesha mapenzi na shauku ya kukutana Naye basi wewe ni katika wale wenye kumpenda kikweli.

Ahmad amepokea katika “al-Musnad” yake na kadhalika at-Tirmidhiy kutoka kwa Mahmuud bin Lubayd ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah akiwapenda watu fulani basi Huwapa mtihani. Ambaye ataridhia basi atapata radhi na ambaye atakasirika basi atapata hasira.”

Dawa yenye kunufaisha ambayo msibiwaji anaweza kutumia ni yeye kukubaliana na Mola Wake kwa yale Anayoyapenda na Kuyaridhia. Sifa ya kipekee ya mapenzi ni mtu kupenda kile mpenzi wake anachopenda. Mwenye kusema kuwa anampenda mpenzi wake halafu akachukia kile mpenzi wake anachokipenda na akapenda kile mpenzi wake anachokichukia basi ameshuhudia dhidi ya nafsi yake mwenyewe ya kuwa anasema uongo na amemfanya mpenzi wake kumkasirikia. Abud-Dardaa´ amesema:

“Pindi Allaah anapoamua jambo Anapenda watu waliridhie.”

´Imraan bin Huswayn amesema alipokuwa katika hali ya kukata roho:

“Ninapenda zaidi kile Anachokipenda zaidi.”

Abul-´Aaliyah alisema baada ya hapo:

“Hiyo ndio dawa na shifaa kwa wale wanaompenda Allaah, lakini sio kila mtu anaweza kujitibu kwa njia hiyo.”

Tazama njia hizi tafauti na jichagulie mwenyewe – Allaah atuongoze sisi na wewe kwa yale Anayoyapenda.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 28
  • Imechapishwa: 14/10/2016