Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:
’Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichinja kondoo wawili weupe wenye pembe, akawachinja kwa mikono yake mwenyewe na akasema: “Bsimillaah” na ”Allaahu Akbar” na akaweka mguu wake juu ya mbavu zao.”[1]
Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.
Hadiyth hii ni dalili ya masuala kadhaa yanayohusiana na Udhhiyah na mukhtasari wa mambo muhimu ni kama ifuatavyo:
1 – Asili ya Udhhiyah ni kuwa imewekwa kwa ajili ya walio hai, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake walikuwa wanachinja kwa ajli ya nafsi zao wenyewe na familia zao. Ama kuitenga kwa ajili ya wafu pekee bila walio hai – kama wafanyavyo baadhi ya watu – hilo halina msingi wowote, isipokuwa kama maiti aliacha anausia, basi wasia huo unatekelezwa. Sunnah ni mtu kuchinja kwa niaba yake na watu wa nyumbani kwake na anaweza kushirikisha maiti wowote katika thawabu zake. Fadhilah za Allaah ni pana.
2 – Dume lina fadhilah zaidi katika Udhhiyah kuliko jike, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichinja madume mawili, kwani nyama yake ni tamu zaidi. Hata hivyo kuchinja jike kunaruhusiwa kwa maafikiano ya wanazuoni.
3 – Inapendeza kuchinja mnyama mwenye pembe kwa kuwa ni bora kuliko asiye na pembe, ingawa asiye na pembe naye inajuzu kumchinja kwa maafikiano.
4 – Inapendeza kuchagua Udhhiyah mzuri kwa umbo na rangi, kwa namna ya kwamba awe mnene na mzuri. Mnyama bora ni yule mweupe sana au mwenye weupe unaozidi weusi. Kufanya hivo ni katika kutukuza nembo za Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ
“Ndivyo hivyo na yeyote anayeadhimisha ´ibaadah za Allaah, basi hayo ni katika uchaji wa nyoyo.”[2]
وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ
“Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa nembo za Allaah.”[3]
Hivyo kutukuza mnyama wa kuchinjwa ni katika kutukuza amri ya Allaah. Ibn ´Abbaas amesema:
“Ni kumchagua mwenye unene, uzuri na ukubwa.”[4]
5 – Inapendeza mtu mwenyewe ajichinjie Udhhiyah yake ikiwa anajua kuchinja, kwa kuwa kuchinja ni ´ibaadah. al-Bukhaariy amesema:
“Abu Muusaa aliwaamuru wasichana zake wachinje kwa mikono yao.”[5]
Ikiwa hawezi kuchinja, basi amuagize muislamu anayejua masharti ya kuchinja na ahudhurie kuchinjwa kwa mnyama wake. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwagiza ´Aliy kuchinja wanyama waliobaki katika hijjah ya kuaga[6].
6 – Yeyote anayependa kuchinja zaidi ya mnyama mmoja, inapendeza kuwachinja siku ya ´Iyd. Kugawanya kwa siku za kuchinja ni jambo linaloruhusiwa na lina manufaa kwa masikini. Kuchinja kunaruhusiwa hadi mwisho wa siku ya 13 ya Dhul-Hijjah, kwa mujibu wa maoni yenye nguvu zaidi ya wanazuoni.
7 – Ni Sunnah kutaja jina la Allaah na kusema “Allaahu Akbar” wakati wa kuchinja. Aseme:
بسم الله ، والله أكبر
”Naaza kwa jina la Allaah, Allaah ni Mkubwa.”
Kutaja jina la Allaah ni wajibu. Kuhusu Takbiyr inapendeza. Haikusuniwa kuongeza maneno mengine kwa kuwa hayakunukuliwa, isipokuwa du´aa ya kukubaliwa. Si Sunnah kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mahali hapa, kwa kuwa si mahali pa kufaa kufanya hivyo.
Ni lazima kutaja jina la Allaah wakati wa kuchinja. Ikiwa kutatokea kusita kwa muda mrefu kabla ya kuchinja, basi lazima arudie kutaja jina la Allaah. Lakini kama kusita ni kwa ajili ya kumwandaa mnyama na kuchukua kisu, basi hilo haliharibu. Inazingatiwa kuwa jina la Allaah litajwe kwa yule anayekusudiwa kuchinjwa. Iwapo atataja jina la Allaah kwa mnyama kisha akamwacha na kwenda kwa mwingine, basi atatakiwa kurudia tena. Lakini kubadilisha chombo cha kuchinjia hakuharibu kutaja jina la Allaah.
[1] al-Bukhaariy (5233) na Muslim (1966).
[2] 22:32
[3] 22:36
[4] Tafsiyr ya Ibn Kathiyr (5/416) na ”Fath-ul-Baariy” (3/536).
[5] Fath-ul-Baariy (10/19).
[6] Ameipokea Muslim kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh).
- Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 30-32
- Imechapishwa: 13/05/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket