Raafidhwah wanajengea hoja kupangusa juu ya miguu kwa kutumia Aayah inayosema:

وَامْسَحُواْ بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَينِ

“… na panguseni vichwa vyenu na miguu yenu hadi vifundoni.”

Wanasoma miguu ambayo ni (وَأَرْجُلِكُمْ) kwa kuiunganisha na kichwa (بِرُؤُوسِكُمْ). Vichwa vinapanguswa. Wanaona kuwa vifundo vya miguu kumekusudiwa kisigino. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wao wanaona kuwa makusudio ya vifundo vya miguu, ni ile sehemu iliyovimba chini ya mguu katika miguu yote mawili. Ni kitendo cha batili kupangusa miguu kwa sababu usomaji wa kawaida wa Aayah (وَأَرْجُلَكُمْ) unakusanya vile viungo vilivyotanguliwa kuoshwa:

وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ

“… nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi… “

Kichwa kilichopanguswa kimetajwa pamoja na viungo vilivyooshwa kwa ajili ya kupangilia, vinginevyo mtu angelifahamu kuwa kichwa kinatakiwa kupanguswa baada ya kuosha miguu.

Kuhusu kisomo kinachosema  (وَأَرْجُلِكُمْ), ni sahihi. Lakini inaweza kujibiwa kwa njia nne:

1 – Kisomo (وَأَرْجُلِكُمْ) ni kwa ajili ya wepesi ili neno liweze kusomwa kirahisi, jambo ambalo linatambulika kwa mujibu wa lugha ya kiarabu.

2 – Makusudio ya kupangusa ni kuosha. Kwa maana nyingine Aayah inaamrisha miguu ioshwe.

3 – Kisomo (وَأَرْجُلَكُمْ) ndio kilichozoeleka na hapo hivyo hakuna utatizi.

4 – Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio ambao wamesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliosha miguu. Haikupokelewa katika Hadiyth hata moja – ijapo dhaifu – ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipangusa miguu yake. Isitoshe hayo hayakuthibiti kutoka kwa Maswahabah zake. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  alimuona mtu mmoja mguuni mwake kuna kijisehemu hakikupata maji ambapo akasema: “Ole visigino kutokamana na Moto!”

Wakati mwingine mtu anachukulia wepesi visigino na pengine visifikiwe na maji.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 184-186
  • Imechapishwa: 04/12/2024