78- ´Aamir bin ´Abdi Qays amesema:

“Kuna Aayah tatu katika Kitabu cha Allaah; sijali nitachokutana nacho asubuhi au jioni pale ninapozikumbuka. Ya kwanza:

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Rahmah yoyote anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake – Naye ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hikmah.” (35:02)

Ya pili:

سَيَجْعَلُ اللَّـهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا

“Allaah atajaalia baada ya dhiki faraji.” (65:07)

Ya tatu:

وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا

“Na hakuna kiumbe chochote katika ardhi isipokuwa riziki yake iko kwa Allaah.” (11:06)

79- Sa´iyd bin ´Abdil-´Aziyz amesema:

“Kulisemwa kuambiwa Abu Usayd al-Fazaariy: Unaishi vipi?” Akasema: “Allaah ni mkubwa na himdi zote anastahiki Allaah. Ataziruzuku nyanyi na nguruwe na asimruzuku Abu Usayd?”

80- Kulisemwa kuambiwa Haatim al-Asamm:

“Ni vipi unajipatia riziki?” Akasema: “Kwa Allaah.” Kukasemwa: “Je, Allaah hukuteremshia dinari na dirham kutoka mbinguni?” Haatim akasema: “Kwani Yeye anamiliki tu mbingu? Ardhi ni Yake na mbingu ni Yake. Ikiwa haniruzuku kutoka mbinguni basi ananiruzuku kutoka ardhini.”

81- Imepokelewa kuwa kuna mtu alimwambia Uways al-Qarniy:

“Ni nani anayekuruzuku?” Akasema: “Ametakasika Allaah! Sikudhani kuwa kuna mtu anayemtambua Allaah kisha aulize juu ya matumizi. Balaa hili limekabiliwa na shaka na ndio maana halinufaishwi na mawaidha.”

82- Abu ´Abdir-Rahmaan al-´Umariy amesema:

“Wakati nilipokuwa kwenye tumbo la mamangu Alikuwa akiniangalia kwa riziki yangu anayoiweka mdomoni kwangu. Nilipokuwa mkubwa na nikajifunza kumtambua Mola wangu ndipo nikaanza kumfikiria vibaya. Kuna kiumbe gani muovu zaidi yangu?”

83- Imesemwa kuwa al-Hasan al-Baswriy amesema:

“Sehemu sabini kwenye Qur-aan nimesoma kuwa Allaah amewadhamini viumbe Wake riziki na sehemu moja tu ndio nimesoma:

الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ ۖ وَاللَّـهُ يَعِدُكُم مَّغْفِرَةً مِّنْهُ وَفَضْلًا

“Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni ufakiri na Allaah Anakuahidini maghfirah kutoka Kwake na fadhila.” (02:268)

Tunatilia shaka maneno ya Mkweli sehemu sabini na kusadikisha maneno ya muongo sehemu moja.”

84- Farqad as-Sabkhiy amesema:

“Katika Tawrat mna: “Ee mwanaadamu! Unapokula riziki Yangu – na ni Mimi ndiye mwenye kuruzuku – ninaziruzuku ndege ndani ya chicha na nyangumi ndani ya bahari.”

85- ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanya kazi kwa ajili ya Allaah na si kwa ajili ya tumbo zenu. Ninakutahadharisheni na dunia na anasa zake. Anasa za dunia kwa Allaah ni uchafu. Ndege za mbinguni zinakuja na kuruka bila ya kuwa na riziki yoyote; hazipandi wala kulima. Pamoja na hivyo zinaruzukiwa na Allaah. Lau mtapinga na kusema kuwa matumbo yenu ni makubwa kuliko ya ndege, basi watazameni wanyama pori, ng´ombe na punda. Wanakuja na kwenda bila ya kuwa na riziki yoyote; hawapandi wala hawalimi. Pamoja na hivyo wanaruzukiwa na Allaah.”

86- ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau mngelimtegemea Allaah ukweli wa kumtegemea basi angelikuruzukuni kama anavyowaruzuku ndege. Wanaruka wakiwa hawana kitu tumboni na wanarudi matumbo yamejaa.”[1]

[1] at-Tirmidhiy (2344).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 58-63
  • Imechapishwa: 18/03/2017