17. Tofauti kati ya ukafiri na kafiri, shirki na mshirikina

Vivyo hivyo ndivo mambo yalivyo kwa kila kilichoitwa kufuru au shirki juu ya wale watu ambao wanaswali kuelekea Qiblah; nayafasiri yote hayo namna hiyo. Kwa sababu tu kumetajwa kufuru na shirki, hakulazimu kuwe na maana ya mtu kutoka nje ya hukumu za Uislamu na kuritadi isipokuwa labda kama inahusiana na kufuru nyingine maalum. Hivyo ndivo yalivyofasiri mapokezi.

28 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa Ja´far bin Burqaan, kutoka kwa Ibn Abiy Nushbah[1], kutoka kwa Anas bin Maalik ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo matatu ni katika msingi wa Uislamu: kumsalimisha mtu anayesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`; hatumkufurishi kwa dhambi na wala hatumtoi nje ya Uislamu kwa sababu ya kitendo, jihaad ni yenye kuendelea kuanzia ile siku Allaah amenitumiliza mpaka pale ambapo mwisho wa ummah wangu watampiga vita ad-Dajjaal; haitofutwa na dhuluma ya mwenye kufanya dhuluma wala uadilifu wa mwenye kufanya uadilifu, na kuamini makadirio yote.”

29 – ´Abbaad bin ´Abbaad ametuhadithia, kutoka kwa as-Swalt bin Diynaar, kutoka kwa ´Uthmaan an-Nahdiy ambaye amesema:

“Niliingia kwa Ibn Mas´uud wakati alipokuwa katika wizara ya fedha Kuufah. Nikamsikia akisema: “Mja haingii ndani ya ukafiri wala shirki mpaka amchinjie asiyekuwa Allaah au amswalie mwengine asiyekuwa Yeye.”[2]

30 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Sufyaan aliyesema:

“Nilikaa jirani na Jaabir bin ´Abdillaah Makkah kwa miezi sita. Bwana mmoja akamuuliza: “Mlimwita yeyote katika wale wanaoswali kuelekea Qiblah kafiri?”  Akajibu: “Ulinzi unaombwa kutoka kwa Allaah!” Akasema: “Mlimwita mshirikina?” Akajibu: “Hapana.”[3]

[1] Jina lake ni Nushbah bin Yaziyd as-Sulamiy na hatambuliki, kama ilivyokuja katika ”at-Taqriyb”. Hadiyth ameipokea Abu Daawuud kupitia kwa Abu Mu´aawiyah.

[2] Athar hiyo n dhaifu mno. as-Swalt bin Diynaar – Abu Shu´ayb al-Hanaaiy al-Baswriy – anajulikana kwa kun-ya yake na ni mwenye kuachwa, kama ilivyo katika ”at-Taqriyb”.

[3] Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh kwa sharti za Muslim.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 04/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy