17. Ni ipi hukumu kwa anayesema kuwa anayeacha kabisa matendo ya dhahiri ni kafiri?

Swali 17: Ni ipi hukumu kwa yule anayesema kwamba mtu anayesema kuwa yule anayeacha kabisa matendo ya dhahiri, jambo ambalo linaitwa na baadhi ya wanazuoni kuwa ni “Jins-ul-´Amal” ni kafiri, na kwamba maneno haya yamesemwa na kundi katika Murji-ah?

Jibu: Sifahamu kwamba maneno haya yamesemwa na Murji-ah, lakini lazima kuwe na matendo, kama ilivyotangulia kuelezwa. Mtu anayekiri shahaadah mbili basi ni lazima afanye matendo. Hii ni kwa sababu maandiko yanayohusiana na kutamka shahaadah mbili na kwamba yule anayetamka shahaadah mbili ni muumini yamefungamanishwa na masharti ambayo hayawezekani pamoja na kuacha matendo kabisa. Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa ni mtakasifu moyoni mwake, ataingia Peponi”.”

Jumla isemayo “hali ya kuwa ni mtakasifu moyoni mwake ” inakanusha shirki, kwa sababu kumtakasia nia Allaah kunapingana na shirki. Mtu anayeacha matendo kabisa ni mshirikina kwa sababu anamuabudu shaytwaan na pia ameipuuza dini ya Allaah. Mwenye kupuuza dini ya Allaah anakufuru. Vilevile Hadiyth nyingine inasema:

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa mtakasifu… ”.”

na:

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa mkweli ndani ya moyo wake… ”.”

na:

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali na kuwa na yakini nayo moyoni mwake… ”.”

na:

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na akakufuru na vile vinavyoabudiwa badala ya Allaah… ”.”

Maandiko haya yanayoeleza kwamba anayetamka shahaadah mbili ni muumini yanafungamanishwa na masharti haya ambayo hayawezekani pamoja na kuacha matendo kabisa. Ni lazima mtu awe anakufuru na kile kinachoabudiwa badala ya Allaah. Aidha asiyefanya matendo basi amepuuza dini ya Allaah, jambo ambalo ni aina mojawapo ya kuritadi. Allaah (Ta´ala):

وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ

“Na wale waliokufuru kwa yale wanayoonywa kwayo ni wenye kukengeuka.”[1]

Kwa hiyo ni lazima mtu afanye matendo. Ikiwa mtu atatamka shahaadah kwa yakini kutoka moyoni mwake na hali ya kuwa hana shaka yoyote, basi ni lazima afanye matendo. Haiwezekani mtu akatamka neno la Tawhiyd kwa ukweli na utakasifu wa nia kisha asiswali kabisa wakati ana uwezo wa kufanya hivyo. Kwa sababu akiacha swalah kunafahamisha juu ya ukosefu wake wa  utakasifu wa nia, ukweli na kwamba moyo wake hauna yakini nayo. Kama moyo wake ungekuwa na yakini nayo, pamoja na utakasifu wa nia na ukweli, basi ni lazima afanye matendo. Ikiwa hatendi matendo yoyote, basi hilo linaonyesha kwamba hana Imani, yakini, utakasifu wa nia, ukweli na kwamba ana shaka na mashaka. Haya yako wazi kutokana na maandiko.

[1] 46:03

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 07/01/2026