5 – Kupangilia. Ni lazima kuosha viungo vya wudhuu´ kwa mpangilio uliotajwa katika Aayah na pia katika matendo yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa kutawadha kwake. Kwa maana nyingine haijuzu kutanguliza kuosha mikono kabla ya uso, kupaka kichwa kabla ya kuosha mikono na kadhalika. Lakini mtu akiosha mkono wa kushoto kabla ya kulia au mguu wa kushoto kabla ya wa kulia, basi wudhuu´ wake ni sahihi kwa maafikiano ya wanazuoni ingawa hilo si jambo bora. Hwafidhw Ibn Hajar amesema:

”an-Nawawiy amesema kwamba kanuni ya Kishari´ah inayoendelea ni kupendelewa kuanza na upande wa kulia katika kila jambo la heshima na upambaji, na kile kilicho kinyume hupendekezwa kuanza na kushoto.” Akasema tena: ”Wanazuoni wameafikiana ya kuwa kuanza na kulia katika wudhuu´ ni Sunnah na anayekiuka hupoteza fadhilah lakini wudhuu´ wake unakamilika.”[1]

Kisha akanukuu kutoka kwa Ibn Qudaamah katika ”alMughniy” ya kwamba amesema:

“Hatujui makinzano yoyote juu ya kutokuwepo wajibu wa kuanza na kulia.”

Shaykh (Rahimahu Allaah) ametoa dalili ya mpangilio kwa Hadiyth:

“Aanzeni na kile ambacho Allaah amekianza nacho.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hivyo alipokuwa ameanza na Swafaa katika kufanya kwake Sa´y. Hadiyth hii kwa tamko la amri imekuja katika ”Sunan-un-Nasaa’iy” (2962) na imo katika ”Swahiyh Muslim” (2950) kwa tamko la khabari, nayo ni kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) katika Hadiyth yake ndefu ya kuelezea namna ya Hijjah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo ndani yake imekuja:

“Alipokaribia Swafaa akasoma:

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ

”Hakika Swafaa na Marwah ni katika Alama za Allaah.”[2]

”Naanza na kile ambacho Allaah amekianza nacho.” Akapanda juu ya Swafaa mpaka akaona Nyumba.”

Tazama ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (1120).

Maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Naanza na kile ambacho Allaah amekianza nacho.”

ni kwamba Allaah alipotaja Swafaa na Marwah alitanguliza Swafaa kabla ya Marwah. Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza na Swafaa katika Sa´y kwa matendo kama Allaah alivyotanguliza kwa kutaja.

[1] Tazama ”Fath-ul-Baariy” (1/270).

[2] 02:158

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 21/05/2026