4 – Kuosha miguu miwili mpaka kwenye vifundo vya miguu

Mtu anatakiwa kueneza maji mpaka kwenye vifundo vya miguu. Kongo mbili za miguu zitaingia katika kuoshwa miguu miwili kama ambavo visugudi vitaingia katika kuoshwa mikono miwili.

Akieneza maji mguuni kutazingatiwa ni mara moja. Ni mamoja amechota mara moja au zaidi ya mara moja. Kinachozingatiwa ni kule kueneza. Vivyo hivyo aoshe mguu wake wa kushoto. Kilicho cha lazima ni mara moja. Mara ya pili na ya tatu ni kitu kimependekezwa.

Inafaa kwa muislamu kutawadha mara mojamoja, mara mbilimbili, mara tatutatu na kwa kutofautisha. Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah):

“Wanachuoni wameafikiana juu ya kwamba jambo la lazima katika kuosha viungo ni mara mojamoja na kwamba mara tatutatu ndio jambo lililopendekezwa. Zimepokelewa Hadiyth Swahiyh juu ya kuosha mara mojamoja, mara tatutatu na kufaa kuosha baadhi ya viungo mara tatutatu, vyengine mara mbilimbili na vyengine mara mojamoja. Wanachuoni wamesema kuwa kutofautisha ni dalili yenye kujulisha kuwa yote hayo yanajuzu na kwamba mara tatutatu ndio kamilifu zaidi na kwamba mara moja kunatosheleza. Kwa hivyo kutofautiana kwa Hadiyth kunafasiriwa kwa njia hiyo.”[1]

[1] Maelezo ya an-Nawawiy juu ya “Swahiyh-ul-Muslim” (03/106)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 14/12/2021