Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

´Abdur-Razzaaq amepokea katika tafsiri yake ya Qur-aan na wengineo ya kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Qur-aan inafasiriwa kwa njia nne: kuna tafsiri ambayo waarabu wanaijua kupitia lugha yao, tafsiri nyingine hakuna yeyote anayepewa udhuru kwa kutoijua, tafsiri ambayo wanaijua wanazuoni peke yao na tafsiri ambayo hakuna aijuaye isipokuwa Allaah pekee; yule mwenye kudai kuijua basi ni mwongo.”

Kama Allaah (Ta´ala) alivosema:

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاء بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Hakuna yeyote anayejua yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho yakiwa ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[1]

MAELEZO

Njia ya kwanza ambayo Qur-aan inatafsiriwa kwayo ni kwa kiarabu, kwa sababu waarabu wamezungumwa kwa lugha hiyo. Isitoshe Qur-aan imeteremshwa kwa lugha hiyo.

Njia ya pili ni ile ambayo hakuna anayesameheka kwa kuijahili, kama mfano wa upwekeshaji na shirki, swalah na swawm, uharamu wa riba, uharamu wa zinaa, uharamu wa mzoga na uharamu wa pombe. Haya ni mambo yaliyo wazi kwa kila mtu, hata watu wa kawaida.

Njia ya tatu ni ile ambayo watu wa kawaida hawaijui, kwa sababu inahitaji kujifunza.

Njia ya nne ambayo hakuna yeyote anayeijua isipokuwa na Allaah ni namna ya majina na sifa Zake, namna ya yaliyomo Peponi na namna ya mambo ya Aakhirah. Haya hayajulikani isipokuwa na Allaah. Yeyote anayodai kuyajua basi ni mwongo. Kama alivosema Allaah (Ta´ala):

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاء بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Hakuna yeyote anayejua yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho yakiwa ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”

Hakuna anayejua namna ya yale ambayo Allaah amewaandalia waja Wake waumini Peponi isipokuwa Allaah pekee. Lakini Allaah ametutajia vitu tunavyovijua kwa ujumla, kama matunda, hariri na asali. Asali tunaijua duniani, lakini asali ya Peponi si kama ya duniani. Maziwa yapo duniani, lakini maziwa ya Peponi si kama ya duniani.

[1] 32:17

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 267-268
  • Imechapishwa: 27/07/2026