160. Allaah na wale waliobobea katika elimu wanajua

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

2 – Tafsiri ya maneno, ni mamoja imeafikiana na udhahiri wake au haikuafikiana na udhahiri wake. Hii ndio istilahi ya wengi katika wafasiri wa Qur-aan na wengineo. Wanaijua tafsiri hii wale wanazuoni waliobobea katika elimu, nayo inaafikiana na kisimamo cha baadhi ya Salaf waliosimama katika maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلاَّ اللّهُ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ

“… na hakuna ajuaye tafsiri zake isipokuwa Allaah na wale wenye msingi madhubuti katika elimu.”

Kisomo hichi kimenakiliwa kutoka kwa Ibn ´Abbaas, Mujaahid, Muhammad bin Ja´far bin az-Zubayr, Muhammad bin Ishaaq, Ibn Qutaybah na wengineo. Kwa maana hiyo visomo vyote viwili ni haki, kama tulivyolizungumzia hilo kwa kina katika maeneo mengine. Kwa ajili hiyo visomo vyote viwili vimenakiliwa kutoka kwa Ibn ´Abbaas, vyote viwil ni haki.

MAELEZO

Hii ndio tafsiri inayojulikana kwa wafasiri wa Qur-aan wa kale kama Ibn Jariyr na wengineo. Wale ambao wamebobea na ambao ni imara katika elimu wanajua tafsiri ya maana hii, kwa ajili hiyo Aayah inasomwa mpaka katika:

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلاَّ اللّهُ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ

“… na hakuna ajuaye tafsiri zake isipokuwa Allaah na wale wenye msingi madhubuti katika elimu.”

Kwa maana wale waliothibiti katika elimu, kwa sababu ubobeaji ni kule kuthibiti. Nao ni wale ambao nyayo zao zimethibiti katika elimu kwa wingi wa elimu yao na uthabiti wao juu ya haki. Tofauti na yule mwenye kujifanya ni msomi; huyu si mwenye kubobea katika elimu. Bali huyumbayumba, kwa sababu bado yuko mwanzo katika kutafuta elimu au anajidai kuwa ni mwanachuoni ilihali si miongoni mwa wale waliobobea katika elimu. Ni jambo limepokelewa kutoka kwa Salaf kwamba walikuwa wakisoma Aayah namna hii:

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلاَّ اللّهُ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ

“… na hakuna ajuaye tafsiri zake isipokuwa Allaah na wale wenye msingi madhubuti katika elimu.”

 Kwa maana nyingine Allaah na wale waliobobea katika elimu pia wanajua zile Aayah zisizokuwa wazi. Visomo vyote viwili ni vyenye kuzingatiwa. Visomo vyote viwili vimepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 260-262
  • Imechapishwa: 23/07/2026