´Abdul-Wahhaab bin ´Abdil-Hakam al-Warraaq, mwalimu wake Abu Daawuud na wengineo, amesema alipozungumzia masimulizi ya Ibn ´Abbaas:

”Fikirini kila kitu, lakini msifikirie kuhusu dhati ya Allaah. Kwani hakika baina ya mbingu hadi kwenye Kursiy Yake kuna nuru elfu saba. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu yake.”

“Mwenye kudai kuwa Allaah yuko hapa, basi ni Jahmiy muovu. Hakika Allaah yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake umezunguka ulimwenguni na Aakhirah.”

´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema:

”Nilimuuliza baba yangu na Abu Zur´ah kuhusu madhehebu ya Ahl-us-Sunnah katika misingi ya dini na madhehebu waliowakuta nayo wanazuoni ulimwenguni kote na ambayo wao wawili wanaitakidi juu ya hilo. Wakasema:

“Tulikutana na wanazuoni Hijaaz, ´Iraaq, Shaam na Yemen na madhehebu yao ilikuwa… Kwamba Allaah (´Azza wa Jall) yuko juu ya ´Arshi Yake na ametengana na viumbe Wake, kama Alivyojieleza Mwenyewe ndani ya Kitabu Chake na kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Halitakiwi kufanyiwa namna. Amekizunguka kila kitu kiujuzi:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[1]

Abu Zur´ah na Abu Haatim ni mfano wa al-Bukhaariy katika kuhifadhi na usahihi.

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema katika ”as-Swahiyh” yake mwishoni mwa mlango dhidi ya Jahmiyyah katika mnasaba wa maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ

“Yeye ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita na ‘Arshi Yake ikawa juu ya maji.”[2]

“Amelingana (استوى) juu ya mbingu maana yake ni kwamba ameinuka juu yake (ارتفع).”

Mujaahid amesema:

“Amelingana (استوى) juu ya mbingu maana yake ni kwamba yuko juu (علا) ya ´Arshi.”

Zaynab, mke wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), amesema:

“Ameniozesha Allaah kutoka juu ya mbingu saba.”[3]

Akaweka mlango kuhusu mengi yanayokanushwa na Jahmiyyah.

Imaam ´Uthmaan bin Sa´iyd ad-Daarimiy amesema:

”Waislamu wamekubaliana kwa kauli moja kuwa Allaah yuko juu ya ´Arshi Yake na juu ya mbingu Zake.”[4]

Amesema mahali pengine:

”Ahl-us-Sunnah wanaamini ya kwamba Allaah kwa ukamilifu Wake yuko juu ya ´Arshi Yake. Anajua na anasikia kutoka juu ya ´Arshi. Hakuna chochote kinachofichikana Kwake kutoka kwa viumbe Wake wala hakuna kitu kinachomzuia kuwaona.”[5]

[1] 42:11

[2] 11:7

[3] al-Bukhaariy (7420).

[4] Naqdhu ´Uthmaan bin Sa´iyd ´alaa al-Mariysiy al-Jahmiy al-´Aniyd, uk. 154.

[5] ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah, uk. 35.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 65-66
  • Imechapishwa: 23/12/2025