Allaah ameshuhudia kuwa amemtuma Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili alinganie Kwake kwa idhini Yake. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا وَدَاعِيًا إِلَى اللَّـهِ بِإِذْنِهِ وَسِرَاجًا مُّنِيرًا

“Ee Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiriaji na mwonyaji na mlinganiaji kwa Allaah kwa idhini Yake na taa lenye kuangaza.”[1]

Allaah amemshuhudilia Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba ni mwenye kutoa ushuhuda dhidi ya watu siku ya Qiyaamah wasije kusema eti hawakujiliwa na mwonyaji. Allaah amewatuma Mitume ili wasimamishe hoja:

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume wenye kutoa bishara njema na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kuletwa ya Mitume.”[2]

Allaah hamuadhibu yeyote isipokuwa baada ya kuwatumia Mitume:

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا

”Hatukuwa Wenye kuadhibu mpaka tumtume Mtume.”[3]

Allaah amemtuma Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kama walivyo ndugu zake wengine – ili atoe ushuhuda dhidi ya watu, kuwabashiria waumini juu ya Pepo na kuwaonya waovu, washirikina na makafiri dhidi ya Moto ikiwa hawatotubia kwa Allaah. Kila Mtume atashuhudia juu ya ummah wake tu ilihali Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atashuhudia juu ya watu wote, kwa sababu ujumbe wake ni wenye kuwaenea wote.

[1] 33:45-46

[2] 4:165

[3] 17:15

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 42
  • Imechapishwa: 28/07/2024