16. Masuala matatu wajibu kwa kila muislamu kuyajua na kuyatendea kazi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akurehemu – kwamba ni wajibu kwa kila m muislamu mwanaume na mwanamke, kujifunza masuala haya matatu na kuyatendea kazi:

MAELEZO

Tambua –  Neno hili tumetangulia kusema kwamba huletwa ili kutilia umuhimu yale yaliyo baada yake. Maana yake ni kwamba jifunze, fahamu na yakinisha.

Allaah akurehemu – Unaombewa du´aa ya rehema. Haya ni kama tulivyotangulia kutaja kwamba mwalimu anatakiwa kumfanyia upole mwanafunzi, amwombee du´aa na ampendezeshee. Kwa sababu hiyo ni miongoni mwa njia kubwa ya kufunza. Hatakiwi kukabiliana na mwanafunzi kwa ususuwavu, ugumu na ukali. Kwa sababu mambo hayo yanakimbiza mbali na elimu. Jengine ni kwamba yanaonyesha jinsi Shaykh (Rahimahu Allaah) anavowatakia wengine kheri na kwamba anataka nasaha, manufaa na maelekezo mazuri.

Ni wajibu – Wajibu ni kitu kinajulikana kwa wanachuoni wa misingi. Wajibu ni kitu ambacho ni lazima. Wanachuoni wa misingi wamekiarifisha kwamba ni kile ambacho analipwa thawabu mwenye kukifanya na haadhibiwi yule mwenye kukiacha. Asili ya wajibu katika lugha ni kuthibiti na kutulizana. Kunasemwa kwamba kitu fulani kimethibiti ikiwa na maana kwamba kimethibiti na kimetulizana. Amesema (Ta´ala) kuhusu mwili:

فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا

“Waangukapo ubavu, basi kuleni kutoka humo.”[1]

Kwa hiyo maneno yake:

“Ni wajibu juu yetu.”

inafahamisha kwamba jambo si kwa njia ya mapendekezo; mwenye kutaka anafanya na mwenye kutaka anaacha. Bali amri ni kwa njia ya ulazima kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Uwajibu huu hautoki kwa Shaykh. Bali unatoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) kwa mujibu wa yale aliyoteremsha katika Qur-aan na Sunnah katika kuwalazimisha waja masuala haya.

Ni wajibu kwa kila muislamu mwanaume na muislamu mwanamke – Bi maana ni lazima kwa kila mume na mke katika waislamu. Ni mamoja ni waungwana, watumwa, wavulana au wasichana. Kwa sababu mwanaume anashirikiana na mwanaume katika mambo mengi ya wajibu isipokuwa yale ambayo dalili zimekuja kumbagua kutokamana na wanaume. Katika hali hiyo yatakuwa yanawahusu wao tu. Mfano wa mambo hayo ni ulazima wa kuswali mkusanyiko misikitini, swalah ya ijumaa, kuyatembelea makaburi na kupambana jihaad katika njia ya Allaah. Mambo haya ni maalum kwa wanaume.

Yale ambayo dalili zimekuja kuonyesha kuwa ni maalum kwa wanaume yatakuwa ni maalum kwao. Vinginevyo wanaume na wanawake wanalingana katika mambo ya uwajibu, kujiepusha na mambo ya haramu na mambo mengine ya ´ibaadah. Miongoni mwa mambo hayo ni kwamba kujifunza elimu ni jambo la lazima kwa wanaume na kwa wanawake. Kwa sababu haiyumkiniki kumwabudu Allaah (Jalla wa ´Alaa) – ambayo Allaah ametuumba kwa ajili yake – isipokuwa kwa kujifunza elimu ambayo kwayo tutajua namna ya kumwabudu Mola wetu. Kitu hicho ni lazima kwa wanaume na kwa wanawake wajifunze mambo ya dini yao na khaswakhaswa mambo yanayohusiana na ´Aqiydah.

[1] 22:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 38-41
  • Imechapishwa: 26/11/2020