16. Du´aa ya kufungulia swalah na maana yake

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada ya hilo kunakuja du´aa ya kufungulia, ambayo ni Sunnah, kwa kusema:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Subhaanak Allaahumma, wa bi Hamdik, wa tabaaraka-smuk, wa ta´alaa Jadduk, wa laa ilaaha Ghayruk.”

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako, ufalme Wako ni mkubwa na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”[1]

Maana ya “Subhaanak Allaahumma” ni kwamba ninakutakasa kutokamana na kasoro zote kwa namna inayolingana na Utukufu Wako.

Maana ya “wa bi Hamdik” ni kuwa Unahimidiwa.

Maana ya “wa tabaaraka-smuk” ni kuwa baraka hufikiwa kwa kutajwa Wewe.

Maana ya “wa ta´ala Jadduk” ni kuwa Utukufu Wako ni Mkubwa.

Maana ya “wa laa ilaaha Ghayruk” ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki katika ardhi wala mbinguni isipokuwa ni Wewe, Allaah.

MAELEZO

Mtu anatakiwa kuanza swalah yake kwa du´aa ya kufungulia swalah. Inasomwa pale tu mtu anapomaliza kuleta Takbiyrat-ul-Ihraam na ni kama ifuatavyo:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako, ufalme Wako ni mkubwa na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”

Hii ndio du´aa fupi ya kufungulia swalah. Ndani yake kote kuna Tawhiyd tupu. Ni nyepesi kwa msomi na ambaye si msomi. Vilevile ni miongoni mwa Hadiyth zilizosihi kabisa. Imepokelewa kupitia njia nyingi kutoka kwa ´Aaishah, Abu Sa´iyd, ´Umar na wengineo (Radhiya Allaahu ´anhum):

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako, ufalme Wako ni mkubwa na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”

Zipo du´aa zengine vilevile za kufungulia swalah. Ukisoma moja katika hizo ni jambo la sawa. Miongoni mwazo ni pamoja vilevile na:

اللَّهُمَّ بَاعِدْ بَيْنِي وَبَيْنَ خَطَايَايَ كَمَا باعَدْتَ بَيْنَ الْمَشْرِقِ والْمَغْرِبِ اللَّهُمَّ نَقِّنِي مِنْ خَطَايَايَ كَمَا يُنَقَّى الثَّوْبُ الأَبْيَضُ مِن الدَّنَسِ اللَّهُمَّ اغْسِلْنِي مِنْ خَطَايَايَ بالثَّلْجِ والْمَاءِ والْبَرَدِ

“Ee Allaah! Nitenge baina yangu mimi na makosa yangu kama ulivyotenga baina ya mashariki na magharibi. Ee Allaah! Nitakase madhambi yangu kama inavyotakaswa nguo nyeupe kutokamana na uchafu. Ee Allaah! Nisafishe kutokamana na madhambi yangu kwa maji, theluji na baridi.”[2]

Wakati mwingine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaweza kufungulia swalah yake kwa du´aa hii, kama alivyopokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

Swali: Ni ipi hukumu ya kukusanya du´aa mbili za kufungulia swalah katika swalah moja? Jibu: Sunnah ni kusoma du´aa moja ya kufungulia swalah. Haikutufikia kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikusanya kati ya du´aa mbili za kufungulia swalah.

Swali: Ni ipi bora kila siku kusoma du´aa aina moja ya kufungulia swalah katika swalah zake zote au bora ni kubadilibadili?

Jibu: Ikiwa ni rahisi bora ni kubadilibadili.

Maana ya “Subhaanak Allaahumma” ni kwamba ninakutakasa kutokamana na kasoro zote kwa namna inayolingana na Utukufu Wako.

Maana ya “wa bi Hamdik” ni kwamba nakusidu pamoja na kukutakasa.

Maana ya “wa tabaaraka-smuk” ni kuwa baraka hufikiwa kwa kutajwa Wewe. Kwa msemo mwingine ni kwamba majina Yake yamefikia ukomo wa baraka. Kila baraka inafikiwa kwa jina la Allaah (Jalla wa ´Alaa), fadhilah na wema Wake.

Maana ya “wa ta´ala Jadduk” ni kuwa Utukufu Wako ni Mkubwa. Utajiri Wako kinachokusudiwa ni ukubwa Wake. Kwa sababu Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) hakuzaa wala hakuzaliwa.

Maana ya “wa laa ilaaha Ghayruk” ni kwamba hakuna mwabudiwa, mbinguni wala ardhini, anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe Mola wetu. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wahHaki na kwamba vile wanavyoomba badala yake ndiyo vya batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[3]

[1] Abu Daawuud (775), at-Tirmidhiy (243) na Ibn Maajah (806). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3/361).

[2] al-Bukhaariy (744) na Muslim (598).

[3] 22:62

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 03/07/2018