80 – ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Tulipewa jukumu la kuwasimamia ngamia. Katika zamu yangu wakati niliporudi jioni baada ya kuwachunga malishoni, nikamkuta Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesimama akiwakhutubia watu. Nilichowahi katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni:

مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَتَوَضَّأُ فَيُحْسِنُ وُضُوءَهُ، ثُمَّ يَقُومُ فَيُصَلِّي رَكْعَتَيْنِ، مُقْبِلْ عَلَيْهِمَا بِقَلْبِهِ وَوَجْهِهِ، إِلَّا وَجَبَتْ لَهُ الْجَنَّةُ

“Hakuna muislamu yoyote atakayetawadha ambapo akafanya vizuri wudhuu´ wake, kisha akasimama na kuswali Rak´ah mbili hali ya kuzielekezea moyo na uso wake, isipokuwa itamthubutukia Pepo.”

Nikasema: “Ni uzuri uliyoje maneno haya!” Ghafla akasema msemaji mmoja: “Yaliyo kabla yake ni mazuri zaidi.” Nikaangalia na kuona kuwa ni ´Umar, ambaye akasema: “Mimi nimekuona ndio punde umefika.” Akasema:

“Hakuna yeyote kati yenu ambaye atatawadha, ambapo akaeneza – au akatimiza – wudhuu´ wake kisha akasema:

أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّداً عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ

“Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume wake.”

isipokuwa atafunguliwa milango saba ya Pepo ambapo ataingia kupitia mlango wowote anaotaka.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Yule mwenye kutawadha kisha akasema:

أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّداً عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ

“Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume wake.”[1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Hizi ni miongoni mwa Hadiyth za matarajio; ya kwamba ambaye atatawadha na kuufanya vyema wudhuu´ wake, kisha akasema Dhikr hii atafunguliwa milango nane ya Pepo ambapo ataingia kupitia mlango wowote anaotaka. Hii ni fadhilah kubwa ya shahaadah mbili. Hata hivyo ni jambo limewekewa sharti ya kujiepusha na madhambi makubwa.

[1] Muslim (234).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 84
  • Imechapishwa: 26/10/2025