Inashauriwa kwa mwalimu awe na bidii katika kuwafundisha. Akitanguliza hilo juu ya manufaa yake ya dunia ambayo si ya dharurah. Aufanye tupu moyo wake wakati wa kukaa kwake kwa ajili ya kuwasomesha kutokana na sababu zote zinazomshughulisha, nazo ni nyingi zinazojulikana. Aidha awe na bidii katika kuwafahamisha. Ampatie kila mmoja wao kile kinachomfaa. Kwa maana kwamba asimzidishe yule asiyeweza kustahimili kuzidishiwa. Asimpunguzie yule anayeweza kuongezewa. Awazoeshe kurudia yale waliyohifadhi. Amsifie yule aliyeonekana kuwa na uelewa mzuri, muda wa kuwa hachelei juu yake fitina ya kujiona au nyingineyo. Yule aliyepunguza amkanye kwa ukali wa upole, muda wa kuwa hachelei kumfukuza mbali. Asimhusudie yeyote miongoni mwao kwa ubora unaoonekana kwake. Asikione kikubwa kile ambacho Allaah (Ta´ala) amemneemesha. Kwani kufanya husuda kwa wageni ni haramu mbaya, tusemeje juu ya mwanafunzi ambaye yuko katika daraja ya mwana? Mwishowe ubora wake unamrejelea mwalimu wake kwa njia ya malipo makubwa huko Aakhirah na sifa njema ulimwenguni.

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 26/08/2026