159. Muislamu anapaswa kutahadhari na kuogopa vichenguzi hivi kumi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hivyo basi, inatakikana kwa muislamu kutahadhari navyo na aviogope juu ya nafsi yake.

MAELEZO

Inatakikana maana yake ni kwamba ni wajibu kwa muislamu kuogopa kutumbukia ndani yake.

Kutahadhari nayo – Bi maana asijitakase nafsi yake. Asiitakase nafsi yake na akasema kuwa yeye anajua na kwamba hana haja ya kujifunza nayo. Wako ambao wanasema kuwa eti watu hawana haja ya Tawhiyd na wanahoji ni kwa nini wanafunzwa waislamu! Wanajiaminisha na khatari. Mtu, midhali bado yuko hai, kuna khatari juu yake akapatwa na mtihani.  Ibraahiym, kipenzi cha Allaah, ambaye aliyavunja masanamu kwa mikono yake na akawekwa ndani ya moto kwa ajili hiyo, amesema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ  رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

“Unikinge mimi na wanangu kuabudu masanamu.” Ee Mola wangu! Hakika hao wamepoteza wengi kati ya watu.” (an-Nahl 14:35-36)

Ibraahiym (´alayhis-Salaam) alichelea juu ya nafsi yake kuhusu ´ibaadah ya masanamu. Kwa sababu nyoyo ziko kati ya widole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma. Mtu anaweza kupinda na kupotea baada ya kuongoka. Mtu asijiaminishe juu ya nafsi yake dhidi ya kupinda na kupotea. Ni wanachuoni wangapi wamepotea na kuangamia? Ni wangapi wenye kumcha Allaah wameingia katika madhambi na kupinda? Maadamu muislamu bado yuhai, basi asijiaminishe nafsi yake kutokamana na fitina na khaswakhaswa wakati fitina ni nyingi:

رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

“Hakika hao wamepoteza wengi kati ya watu.”

Aviogope juu ya nafsi yake – Anatakiwa kuviogopa na wala asiiaminishe nafsi yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 201-202
  • Imechapishwa: 20/03/2019