Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kundi la tatu ni wale wanaofuata ujinga, nalo lina wengi miongoni mwa wale wanaojinasibisha na Sunnah na kuwafauta Salaf.

MAELEZO

Hawa wanasema kuwa Salaf, wanazuoni bali hata Mitume walikuwa wajinga kuhusu maana ya majina na sifa za Allaah. Kwa mujibu wao ni kwamba walikuwa wakitamka matamshi bila ya kujua maana yake. Walimtegemezea Allaah maana yake na kuamini kuwa hiyo ndio ilikuwa ´Aqiydah ya Salaf. Ndiyo maana husema kuwa Allaah ndiye anajua zaidi makusudio Yake.

´Aqiydah hii ni kosa kubwa, kwa sababu maana yake ni kwamba Allaah ametuteremshia maandiko tusiyoyajua, jambo ambalo linapingana na maneno Yake (Ta´ala):

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayah zake na ili wapate kukumbuka wale wenye akili.”[1]

Allaah alituamrisha tuzitafakari Aayah za Qur-aan, ambapo zilizo kubwa zaidi ni Aayah za majina na sifa za Allaah ambazo ni kubwa kuliko Aayah za hukumu. Allaah ameamrisha kuzitafakari. Ikiwa maana zake hazieleweki, basi kuna faida gani ya kuzitafakari? Tutafakari kitu tusichokifahamu? Hapo itakuwa Allaah anatulazimisha lisilowezekana. Isitoshe Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ

”Je, hawakuzingatia maneno?”[2]

Bi maana Qur-aan. Hii ni karipio kutoka kwa Allaah kwa wale wasiolitafakari. Kwa nini waitafakari Qur-aan ikiwa haieleweki? Bali Allaah amesema:

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا

“Je, hawaizingatii Qur-aan au nyoyoni mwao mna kufuli?”[3]

Hakubagua kitu katika Qur-aan kwamba kisizingatiwe. Abu ´Abdir-Rahmaan as-Sulamiy amesema:

“Wale ambao walikuwa wakitusomesha Qur-aan – ´Uthmaan bin ´Affaan, ´Abdullaah bin Mas´uud na wengineo – wametueleza kwamba: “Baada ya kuhifadhi Aayah kumi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), tulikuwa hatuzivuki mpaka tujifunze elimu yazo na kuzitendea kazi.” Tukajifunza Qur-aan, elimu na matendo.”[4]

Mujaahid amesema:

“Nimeisoma Qur-aan yote mara tatu mbele ya Ibn ´Abbaas; nikisimama katika kila Aayah na nikimuuliza kwayo.”

Hakuzungumzia baadhi ya Aayah; bali ”kila Aayah”. Kwa hiyo kusema kuwa kuna sehemu ya Qur-aan isiyotafakariwa ni ´Aqiydah iliyo wazi ubatilifu wake. Kuinasibisha kwa Salaf ni uongo na uzushi. Hii sio ´Aqiydah ya Salaf. Kwa hiyo inawajibika kutanabahi jambo hili, kwa sababu ´Aqiydah hii ni khatari sana. Aidha kujinasibisha kwao na Sunnah na Salaf si sahihi.

[1] 38:29

[2] 23:68

[3] 47:24

[4] Ahmad (5/410).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 254-256
  • Imechapishwa: 22/07/2026