154. Jambo baya zaidi kuliko kukanusha Kufufuliwa

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Tawraat imejaa sifa zinazolingana na sifa zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Hadiyth. Wala ndani yake hakuna maelezo ya wazi kuhusu Kufufuliwa kama yalivyo katika Qur-aan. Kwa hiyo ikiwa inafaa kuzipindisha maana sifa ambazo vitabu viwili vimekubaliana juu yake, basi Kufufuliwa kuna haki zaidi ya kupindishwa maana ambako kumetajwa na kimoja wapo. Na ni jambo linalotambulika vyema kabisa katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba kupindisha maana hilo jambo la pili ni batili, basi la kwanza lina haki zaidi kuwa batili.

MAELEZO

Kwa sababu Tawraat na Qur-aan vyote viwili ni kutoka kwa Allaah. Kwa hivyo vyote viwili vinawafikiana. Tawraat imejaa kutajwa majina na sifa za Allaah kama ilivyo ndani ya Qur-aan. Mu´tazilah wamekanusha majina na sifa za Allaah, ilihali yaliyomo katika Qur-aan kuhusu Kufufuliwa ni mengi zaidi kuliko yaliyomo ndani ya Tawraat kuhusu Kufufuliwa. Hapana shaka yoyote kwamba kukanusha Kufufuliwa ni batili. Lakini ni jepesi zaidi kuliko kukanusha majina na sifa za Allaah, ingawa yote mawili ni batili. Lakini batili hutofautiana; baadhi yake ni mbaya zaidi kuliko nyingine. Hivyo kukanusha majina na sifa za Allaah ni kosa kubwa zaidi kuliko kukanusha Kufufuliwa.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 253
  • Imechapishwa: 22/07/2026