153. Maelezo yaliyokubaliwa na yaliyokaripiwa

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kadhalika ni jambo linalotambulika kwamba aliwasema vibaya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) watu wa Kitabu kwa yale waliyoyapotosha na kuyabadilisha. Aidha inatambulika vyema kwamba kwamba Tawraat imejaa kutajwa sifa za Allaah. Hivyo lau jambo hili lingekuwa miongoni mwa yale yaliyopotoshwa na kubadilishwa, basi kuwakemea juu ya hilo kungekuwa ni jambo la kwanza zaidi. Vipi iwe hivyo, hali ya kuwa walipokuwa wakitaja sifa za Allaah mbele yake, basi alikuwa akicheka kwa kuwashangaa na kuthibitisha sifa za Allaah[1]? Hakuwahi kabisa kuwakosoa kwa yale ambayo wanaokanusha sifa huwakosoa wenye kuthibitisha sifa, ikiwa ni pamoja na wenye kufanya kiwiliwili na ufananishaji. Bali walikosolewa kwa kusema:

يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ

”Mkono wa Allaah umefumbwa.”[2]

إِنَّ اللَّـهَ فَقِيرٌ وَنَحْنُ أَغْنِيَاءُ

”Hakika Allaah ni fakiri na sisi ni matajiri.”[3]

Pia kutokana na imani yao kuwa Allaah alipumzika baada ya kuumba mbingu na ardhi:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ

“Hakika Tumeumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yake katika siku sita na wala hatukuguswa na uchovu wowote.”[4]

MAELEZO

Allaah aliwakosoa mayahudi na manaswara kwa kupotosha Tawraat na Injiyl, lakini hakuwakosoa kwa kuthibitisha majina na sifa za Allaah, kwa sababu hawakuyapotosha. Bali walipotosha mambo mengine.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwakosoa mayahudi kwa kuthibitisha kwao majina na sifa za Allaah kama Jahmiyyah na Mu´tazilah wanavyowakosoa Ahl-us-Sunnah kwa kuthibitisha majina na sifa za Allaah. Hakuwatuhumu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mayahudi kuwa ni wenye kumfanya Allaah kuwa na kiwiliwili pale waliposema kuwa Allaah atazikamata mbingu na ardhi kwenye mkono Wake wa kuume:

وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

”Ardhi yote itawekwa mkononi Mwake siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.”[5]

Ikafahamisha kwamba ´Aqiydah yao ni sahihi. Aliwakubalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´Aqiydah yao kwamba Allaah anao mkono, lakini aliwakaripia pale waliposema:

يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ

”Mkono wa Allaah umefumbwa.”

إِنَّ اللَّـهَ فَقِيرٌ وَنَحْنُ أَغْنِيَاءُ

”Hakika Allaah ni fakiri na sisi ni matajiri.”

Kwa maana kwamba Allaah anatuomba swadaqah. Hii inaonesha kuwa Allaah ni fakiri na sisi ni matajiri. Walisema hivo kwa ajili ya kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vinginevyo wao wanajua kwamba Allaah ni Mkwasi na wanajua kwamba Allaah Ameamrisha zakaah na swadaqah. Lakini walitaka kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumchezea shere.

Aidha aliwakosoa kwa ´Aqiydah yao kwamba Allaah alipumzika siku ya saba baada ya kuwaumba viumbe. Allaah akawaraddi kwa hilo na kusema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ

“Hakika Tumeumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yake katika siku sita na wala hatukuguswa na uchovu wowote.”

Hakuwaraddi kwa kuthibitisha kwao majina na sifa za Allaah; bali Aliwaraddi kwa kuthibitishia Allaah (´Azza wa Jall) mapungufu.

[1] al-Bukhaariy (8/423) na Muslim (2786).

[2] 5:64

[3] 3:181

[4] 50:38

[5] 39:67

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 251-253
  • Imechapishwa: 22/07/2026