Wako miongoni mwa watu ambao wanakataa kukubali elimu inapofikishwa kwa sababu ya kiburi juu ya haki na kuirudisha haki. Huyu atakuwa pamoja na wenye kufanya kiburi. Hii ni kufuru ya kufanya kiburi juu ya haki.

Miongoni mwa watu kuko ambao wanakataa kujifunza dini kwa ajili ya kutokuwa na hamu nayo na kiupuuza, huyu anakuwa pamoja na wenye kugengeuka. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ

”Wale waliokufuru wanapuuza yale wanayoonywa.” (al-Ahqaaf 46:03)

Miongoni mwa watu wako ambao wanakataa dalili na wanakataa kukubali haki pindi wanapobainishiwa kwa ajili ya kulinda dini ya mababa zao na mababu zao na kasumba. Hakuwakubali haki, afadhali abaki kwa yale aliyomo na aliyokuta nayo wakiyafanya mababa na mababu zake, kama walivokuwa washirikina tokea zamani hadi hivi sasa.

Wale wanaoabudu makaburi hawakubali haki na wala hawakubali kujadiliwa. Ni wenye kukinaika kabisa juu ya yale waliyomo. Hawakubali maelekezo na miongozo. Wameyaziba masikio yao dhidi ya kukubali haki na wanaendelea juu ya yale waliyomo. Bali wakati mwingine huenda hata wakapambana kwa ajili ya hilo na wakajitolea nafsi zao kwa sababu ya itikadi hii batili. Hawakubali haki vovyote watavyosikia Qur-aan, Sunnah, makatazo ya shirki na maamrisho ya Tawhiyd na wala hawajali haya. Bali wameyapuuza. Huku ni kukengeuka dhidi ya dini sahihi na kuridhika na dini batili. Haya yanapatikana kwa watu wengi hii leo. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ آمَنُوا بِالْبَاطِلِ وَكَفَرُوا بِاللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ

”Wale walioamini ubatilifu na wakamkufuru Allaah, basi hao ndio waliokhasirika.” (al-´Ankabuut 52)

Watu hawa wanaamini ubatilifu na wanamkufuru Allaah. Wanamuabudu na kumuomba asiyekuwa Yeye, wanatafuta uokozi kutoka kwa wengine, wanaonelea kufanyiwa ´ibaadah mwingine badala ya Allaah na wanamkufuru Allaah. Wanafanya hivo waziwazi na hadharani. Huku ndio kukengeuka. Ni kasumba. Wakati Abu Twaalib alipokuwa anataka kukata roho, kama mnavojua kusimama kwake bega kwa bega pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ulinganizi wake, kumhami kwake na kuhami ulinganizi  wake, lakini hata hivyo hakuingia katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja kumlingania hali ya kumuonea huruma wakati alipokuwa anakataka kukata roho ambapo akamwambia:

“Ewe ami yangu! Sema ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah`. Ni neno ambalo nitakutetea kwalo mbele ya Allaah. Walikuwepo watu katika washirikina ambao wakamwambia: “Hivi kweli unataka kuiacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Walitambua kuwa akisema ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah`, basi atakuwa ameiacha dini ya ´Abdul-Muttwalib ambayo ni ya kuabudu masanamu. Akamrudilia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia vilevile na wale wengine wakamwambia tena: “Hivi kweli unataka kuiacha dini ya ´Abdul-Muttwalib?” Mwishowe akakubali kuwa yeye yuko katika dini ya ´Abdul-Muttwalib na akakataa kusema ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah` na akafa juu ya hayo. Kasumba ya kung´ang´ania dini ya ´Abdul-Muttwalib na kukengeuka kukubali Tawhiyd. Matokeo yake akawa ni mtu wa Motoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nitakuombea msamaha kwa Allaah midhali sijakatazwa.” Ndipo Allaah akateremsha:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ

”Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwaombee msamaha washirikina, japokuwa ni jamaa zao wa karibu, baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa Motoni.” (at-Tawbah 09:113)

Pia akateremsha kuhusu Abu Twaalib:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

”Hakika wewe huwezi kumwongoza umpendaye, lakini Allaah humwongoza amtakaye; Naye ndiye mjuzi zaidi ya waongokao.” (al-Qaswasw 28:56)

Kuliingia watu watatu msikitini na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anawahadithia Maswahabah zake. Mmoja wa wale watu watatu akaja na akaa katika ule mzunguko wa elimu akiwa na shauku ya kutaka kujifunza. Mtu wa pili akaona haya kuondoka na hivyo akaja kukaa. Mtu wa tatu akapuuza na akaondoka nje. Mtume akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, nisikujuzeni kuhusu khabari za watu watatu?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah!” Ama wa kwanza wao amesogea ambapo Allaah akamwingiza katika rehema Zake, wa pili ameona haya na Allaah akamuonea haya na wa tatu amepuuza na Allaah Naye akampuuza.”[1]

Haya ndio malipo ya wale wenye kupuuza juu ya kujifunza mambo ya dini yao.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (66), Muslim (2176) na at-Tirmidhiy (2724).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 193-195
  • Imechapishwa: 14/03/2019