Swali 15: Baadhi wanafikiri kuwa ni wanazuoni tu ndio wanatakiwa kulingania katika dini ya Allaah na wengine hawahitajii kulingania kutokana na yale waliyojifunza. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Huu sio ufikiriaji. Huu ndio uhakika wa mambo. Wanazuoni tu ndio wanatakiwa kulingania. Mimi pia nasema hivo. Lakini kuna mambo yako wazi yanayojulikana na watu wote. Kila mtu aamrishe mema na kukataza maovu kwa kiasi cha elimu yake. Aiamrishe familia yake swalah na mambo mengine yaliyo wazi. Hili ni wajibu hata kwa wasiokuwa wasomi. Wanatakiwa kuwaamrisha watoto wao kuswali msikitini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waamrisheni watoto zenu kuswali pindi wana miaka saba na wapigeni kwayo pindi wana miaka kumi na muwatenganisha kwenye vitanda.”[1]

“Nyote ni wachungaji na kila mmoja ataulizwa kwa kile alichokichunga.”[2]

Huku kunaitwa kuchunga. Kunaitwa kuamrisha mema na kukataza maovu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote yule mwenye kuona maovu, basi ayabadilishe kwa mkono wake. Ikiwa hawezi, ayabadilishe kwa mdomo wake. Ikiwa hawezi, ayabadilishe kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu.”[3]

Mtu wa kawaida anapaswa kuiamrisha familia yake na wengine kuswali, kutoa zakaah, kumtii Allaah na kujiepusha na maasi. Aidha aisafishe nyumba yake na madhambi na awalee watoto wake juu ya utiifu. Hili linampasa hata kama si msomi. Kwa sababu yanajulikana na kila mtu; hili ni jambo liko wazi.

Ama kuhusu fataawaa, ya halali na ya haramu, shirki na Tawhiyd, wanazuoni tu ndio wanayasimamia hayo.

[1] Abu Daawuud (495). Hadiyth ni Swahiyh. Tazama ”Nasb-ur-Raayah” (1/298) kwa tamko kama hilo.

[2] al-Bukhaariy (853).

[3] Muslim (49).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy