15. Ni ipi hukumu ya watu wanaochukulia wepesi jambo la swalah?

Swali 15: Watu wengi hii leo wanaichukulia wepesi swalah na baadhi yao wanaiacha kabisa. Ni ipi hukumu ya watu hawa? Ni lipi la wajibu kwa muislamu juu yao na khaswa wale ndugu kama vile baba, mtoto, mke na wengineo?

Jibu: Kuchukulia wepesi swalah ni katika maovu makubwa na ni miongoni mwa sifa za wanafiki. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu.”[1]

Vilevile amesema kuhusu sifa zao:

وَمَا مَنَعَهُمْ أَن تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَبِرَسُولِهِ وَلَا يَأْتُونَ الصَّلَاةَ إِلَّا وَهُمْ كُسَالَىٰ وَلَا يُنفِقُونَ إِلَّا وَهُمْ كَارِهُونَ

”Haikuwazuilia kukubaliwa michango yao isipokuwa kwa kuwa wao walimkufuru Allaah na Mtume Wake na wala hawaiendei swalah isipokuwa wao huwa katika hali ya uvivu na wala hawatoi isipokuwa wakiwa wamechukia.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah nzito zaidi kwa wanafiki ni swalah ya ´Ishaa na swalah ya Fajr. Endapo wangelijua yale yanayopatikana ndani yake basi wangeziendea ijapo kwa kutambaa.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kwa hivyo ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na muislamu wa kike kuzichunga zile swalah tano ndani ya wakati wake, kuziswali kwa utulivu, kuzielekea, kuenyenyekea ndani yake na kuhudhurisha moyo. Amesema (Ta´ala):

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[3]

Vilevile kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alimwamrisha yule ambaye aliswali vibaya kuirudia swalah yake.

Ni lazima kwa wanamme peke yao waihifadhi kwa mkusanyiko pamoja na ndugu zao katika nyumba za Allaah ambazo ni misikiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesikia wito na asiuitikie, basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”

Ameipokea Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy, Ibn Hibbaan na al-Haakim kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliulizwa: “Ni upi udhuru?” Akasema:

“Khofu au maradhi.”

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Alijiwa na bwana mmoja kipofu akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mimi anayeniongoza kuelekea msikitini. Je, nina ruhusa ya kuswalia nyumbani kwangu?” Akampa ruhusa. Kisha baadaye akamwita na kumuuliza: “Je, unasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akamwambia: “Basi imewajibika.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimetamani niamrishe kuswaliwe ambapo ikasimamishwa kisha nikamwamrisha mtu awaswalishe watu halafu nikaondoka na kikosi cha wanamme walio na vifurushi vya kuni kuwaendea watu ambao hawashuhudii swalah nikazichoma nyumba zao kwa moto.”

Hadiyth hizi Swahiyh zinajulisha kuwa kuswali kwa mkusanyiko kwa wanamme ni katika mambo muhimu mno na kwamba yule mwenye kujiacha nyuma anastahiki adhabu ya kumkomesha. Namuomba Allaah azitengeneze hali za waislamu wote na awatunuku tawfiyq kwa yale yanayowaridhisha.

Kuhusu kuacha swalah kabisa, ijapo ni katika baadhi ya nyakati, ni ukafiri mkubwa. Haijalishi kitu hata kama anakiri uwajibu wake kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Ni mamoja ambaye ameiacha ni mwanamme au mwanamke. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri na shirki ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Zipo Hadiyth nyinginezo nyingi kuhusu maudhui hayo.

Kuhusu anayekanusha ulazima wake, katika wanamme au wanawake, basi anakufuru ukafiri mkubwa kwa maafikiano ya wanazuoni. Haijashi kitu hata kama ataswali. Tunamuomba Allaah atusalimishe waislamu wote kutokamana na jambo hilo. Kwani hakika Yeye ni mbora wa kuombwa.

Ni lazima kwa waislamu wote kupeana nasaha na kuusiana kwa haki na kusaidiana juu ya wema na kumcha Allaah. Katika hayo kunaingia vilevile kumnasihi yule anayekosa swalah ya mkusanyiko au anaichukulia wepesi ambapo akaiacha katika baadhi ya nyakati na pia kumtahadharisha juu ya ghadhabu na adhabu ya Allaah. Aidha ni lazima kwa baba yake, mama yake, ndugu zake na watu anaoishi nao nyumba moja wamnasihi na waendelee juu ya jambo hilo mpaka amwongoze Allaah na kunyooka. Vivyo hivyo inahusiana na yule anayeichukulia wepesi au anaiacha upande wa wanawake. Ni lazima kuwanasihi na kuwatahadharisha na ghadhabu na adhabu ya Allaah, kuendelea juu ya jambo hilo, kumsusa ambaye hatekelezi na kumtia adabu inayoendana naye ikiwa watu wanaweza kufanya hivo. Kwa sababu kufanya yote hayo ni katika kusaidiana juu ya wema na kumcha Allaah na kuamrishana mema na kukataza maovu, jambo ambalo Allaah ameliamrisha juu ya waja Wake wanamme na wanawake. Amesema (Subhaanah):

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah na wanamtii Allaah na Mtume Wake – hao Allaah atawarehemu. Kwani hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapokuwa na miaka saba  na wapigeni kwayo wanapofikisha miaka kumi na pia watenganisheni katika malazi.”

Ikiwa watoto wa kiume na watoto wa kike wanaamrishwa swalah wanapofikisha miaka saba na wanachapwa wanapofikisha miaka kumi, basi ambaye amekwishabaleghe ana haki zaidi ya kuchapwa inapokuja katika ulazima wa kuswali na kuchapwa kwa ajili yake wanapoiacha pamoja na nasaha zenye kuendelea. Sambamba na hilo wanaoamrisha wanatakiwa kunasihiana kwa haki na kufanya subira juu yake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanadamu bila shaka yumo katika khasara, isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa haki na wakausiana subira.”[5]

Yule ambaye ataacha swalah baada ya kubaleghe na asikubali nasaha lipelekwe jambo lake katika mahakama yanayohukumu kwa Shari´ah ili wamtake kutubia. Akitubia ni vizuri na vinginevyo atauliwa. Tunamuomba Allaah azitengeneze hali za waislamu, awatunuku ufahamu katika dini, awawafikishe katika kusaidiana juu ya wema na kumcha Allaah, kuamrishana mema na kukataza maovu, kunasihiana kwa haki na kufanya subira juu yake. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa na Mkarimu.

[1] 04:142

[2] 09:54

[3] 23:01-02

[4] 09:71

[5] 103:01-03

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 14-19
  • Imechapishwa: 15/08/2022