Swali 15: Ni ipi hukumu ya kupangusa juu ya kilemba?

Jibu: Ni jambo limethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufuta juu ya kilemba. Kimtazamo kilemba kina haki zaidi ya kupanguswa kuliko kupangusa juu ya soksi za ngozi kwa sababu kinavaliwa juu ya kitu ambacho tayari kimeshafutwa. Usafi wa kiungo hichi, bi maana kichwa, ni nyepesi zaidi kuliko usafi wa miguu kwa sababu usafi wa kichwa unakuwa kwa kupangusa. Sehemu ya kichwa, ambayo ni kile kilemba, ina haki zaidi ya kupanguswa kuliko vazi lililovaliwa kwenye kiungo kinachooshwa.

Je, kupangusa juu ya kilemba kunashurutishwa yaleyale yanayoshurutishwa juu ya soksi za ngozi? Je, ni lazima kwa mtu akivae akiwa na twahara? Je, muda wake ni mchana mmoja na usiku wake kwa ambaye ni mkazi na michana mitatu na nyusiku zake kwa ambaye ni msafiri? Au inafaa kupangusa moja kwa moja pasi na kuzingatia mtu amekivaa akiwa na twahara na muda uliopangwa isipokuwa tu katika hadathi kubwa hakipanguswi kwa sababu mtu anatakiwa kuosha mwili mzima? Wanazuoni wametofautiana juu ya jambo hili.

Wale wanaosema kwamba kufuta juu ya kilemba hakukushurutishwa sharti zozote wanajengea hoja kwamba hakuna dalili yoyote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanasema kuwa kukilinganisha na soksi za ngozi ni ulinganisho wa kimakosa kwa sababu soksi za ngozi zinakuwa kwenye kiungo kilichooshwa na kilemba kinakuwa katika kiungo kilichopanguswa na hivyo twahara yake ni nyepesi. Kwa ajili hiyo hawashurutishi sharti zozote. Lakini hapana shaka kwamba bora ni kusimama katika upande salama zaidi.  Jambo jenyewe ni nyepesi. Mtu ahakikishe amevaa kilemba akiwa katika hali ya twahara, akivue unapomaliza ule muda uliowekwa wa kupangusa, afute kichwa chake kisha akivae tena.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/169)
  • Imechapishwa: 06/05/2021