68- Kisha ataondoka kwenda ´Arafah na akae kwenye mawe chini ya mlima wa Rahmah akiwa na wepesi wa kufanya hivo. Vinginevyo anaweza kusimama kokote ´Arafah.

69- Asimame kwa kuelekea Qiblah hali ya kuinyanyua mikono yake, aombe du´aa na kuleta Talbiyah.

70- Aseme “Laa ilaaha illa Allaah” kwa wingi”. Kwani ndio du´aa bora siku ya ´Arafah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Bora niliyosema mimi na Mitume wengine siku ya ´Arafah ni:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa pekee hana mshirika. Ufalme ni Wake, himdi ni Zake Naye juu ya kila jambo ni muweza.”[1]

71- Wakati fulani itafaa kwake kuzidisha katika Talbiyah kwa kusema:

إنما الخير خير الآخرة

“Hakika kheri khaswa ni kheri ya Aakhirah.”[2]

72- Sunnah kwa ambaye amesimama ´Arafah ni yeye kutokufunga siku hii.

73- Aendelee katika hali hii hali ya kuwa ni mwenye kumtaja Allaah, kuleta Talbiyah na akiomba ayatakayo na huku akitaraji kutoka kwa Allaah (Ta´ala) amjaalie kuwa miongoni mwa wale Anaowaacha huru na ambao Malaika hujifakharisha nao, kama ilivyokuja katika Hadiyth:

“Hakuna siku ambayo Allaah huwaacha watu huru kutokamana na Moto kama siku ya ´Arafah. Hakika Hukaribia kisha akajifakharisha kwao Malaika na kusema: “Wanataka nini watu hawa?”[3]

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Allaah hujifakhari kwa watu wa ´Arafah watu wa mbinguni na anasema: “Watazameni waja Wangu; wamenijia wakiwa timtim na wenye mavumbi.”[4]

Aendelee katika hali hiyo mpaka jua lizame.

[1] Hadiyth ima ni Swahiyh au nzuri. Ina njia nyingi zilizotajwa katika “as-Swahiyhah” (1503).

[2] Hilo limethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyobainishwa katika “asili”.

[3] Ameipokea Muslim na wengineo. Tazama ”at-Targhiyb” (2/129).

[4] Ameipokea Ahmad na wengineo. Wameisahihisha kundi, kama nilivyobainisha katika ”Takhriyj-ut-Targhiyb”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 29
  • Imechapishwa: 15/07/2018