149. Hawakuinusuru Sunnah na wala hawakuivunja batili

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kundi linalofata mawazo linasema kuwa makusudio ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutaka watu waamini batili juu ya yale maandiko yanayozungumzia sifa; alikusudia kwayo maana na hakuwabainishia maana hiyo. Alichotaka ni wao wenyewe wafikirie na waijue haki kwa kutumia akili yao Kisha baada ya hapo wajitahidi kugeuza maandiko hayo kutoka katika majulisho ya maana yake. Kwa maana nyingine lengo ni kuwatia kwenye mtihani na kuwakalifisha wahangeike kuyageuza maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika majulisho ya maana yake na muqtadha yake na hivyo waitambue haki kwa njia nyingine. Haya ndio maoni ya wanafalsafa, Jahmiyyah, Mu´tazilah na wengine wenye maoni kama hayo.

Watu hawa ndio ambao tumekusudia kuwaraddi katika fatwa hii kwa sababu ni jambo linalotambulika kuwa watu ni wenye kuwakimbia wale watu wa sampuli ya kwanza tofauti na hawa wa mwisho. Kwa sababu watu hawa mara nyingi ni wenye kujionyesha kuwa wanainusuru Sunnah, ilihali ukweli wa mambo ni kwamba hawakuinusuru Sunnah wala hawakuwavunja wanafalsafa. Lakini wanafalsafa wamewalazimisha kusema juu ya Aakhirah yale waliyosema kuhusu maandiko ya sifa. Hoja yao dhidi yao waliwaambia kuwa wanajua kwa yakini kuwa Mitume wamefikisha ujumbe kuhusu Kufufuliwa kwa miili na tunajua ubovu wa shubuha inayopingana na ´Aqiydah hii.

MAELEZO

Kundi la pili ni wale wenye kupindisha maana. Nao ndio ambao Shaykh (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu hiki kuwaraddi. Nao ni wale wanaosema kuwa majina na sifa za Allaah hazitakiwi kufasiriwa juu ya maana zake za wazi, kwa sababu eti maana ya wazi inapelekea ufananishaji. Kwa hiyo huzigeuza kwenda katika maana nyingine ambazo kwa madai yao hazina ufananishaji. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja na Maandiko haya, lakini kwa madai yao hakutaka watu wayaamini juu ya maana zake za wazi, bali alitaka wayafasiri kutoka katika maana zake za wazi, kwa sababu eti maana yake ya wazi haimstahikii Allaah. Maana ya jambo hili ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja na mafumbo na vitendawili na wala hakuja na maneno faswaha. Hali ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mjuzi zaidi wa viumbe, mfaswaha zaidi wa viumbe na mtu mwenye kuwatakia watu kheri zaidi. Hivyo huku ni kumtuhumu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba hakufikisha wala hakuwabainishia watu maana iliyokusudiwa katika yale aliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wake.

Wapindisha maana katika Jahmiyyah, Mu´tazilah na waliowafuata mrengo wao ndio wenye kuraddiwa hapa. Ni wale wanaopindisha maana ya majina na sifa za Allaah kutoka katika maana zake halisi. Ama yale mawili mengine – wale wanaofuata mawazo na wanaofuata ujinga – wanaraddiwa katika vitabu vingine.

Watu huwakimbia wale wanaofuata mawazo na wanafalsafa. Lakini wale wanaopindisha maana huwadanganya watu kwamba wao ni wanazuoni na hudai kuwa wanainusuru Sunnah na kuwajibu watu wa upotofu. Kwa hiyo khatari yao juu ya waislamu ni kubwa zaidi kuliko khatari ya wengine. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba hawakuinusuru Sunnah na wala hawakuwasambaratisha wanafalsafa, ksababu hawakuwaraddi kwa Qur-aan na Sunnah. Bali waliwaraddi kwa elimu ya mantiki na elimu ya falsafa. Jambo hili halinusuru Uislamu wala halisambaratishi batili – bali huzidisha shari juu ya shari. Hivyo anayewajibu watu wa upotofu kwa kitu kisicho Shari´ah na ambacho hakuja nacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hasaidii chochote, bali huzidisha jambo kuwa baya zaidi, kwa sababu watu hutofautiana katika akili na mitazamo yao. Wakati walipowaraddi Baatwiniyyah ambao walikanusha kufufuliwa na kurejeshwa baada ya kufa na kusema kuwa maneno ya Allaah kuhusu kufufuliwa na kurejeshwa hayako juu ya maana yake ya dhahiri wala hakuna kufufuliwa, hakuna Pepo wala Moto na wakawaambia watu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizua mambo hayo kwa ajili ya maslahi ya watu, Baatwiniyyah wakawaambia kuwa wote wawili wamepindisha maana; wao wamepindisha maana ya Maandiko ya Kufufuliwa na Kurejeshwa na kwamba wao wamepindisha maana ya Maandiko ya majina na sifa za Allaah. Zingatia pia kwamba majina na sifa yametajwa ndani ya Qur-aan zaidi kuliko kutajwa Kufufuliwa. Kwa nini kupindisha kwenu maana kuwe halali na kupidisha kwetu maana kuwe batili? Kwa nini wanawaraddi Baatwiniyyah ilihali wao ndio wapotovu zaidi? Baatwiniyyah wakawaambia Mu´tazilah kwamba Mitume wamekuja kuthibitisha Kufufuliwa na pia wamekuja kuthibitisha majina na sifa za Allaah; kundi la kwanza wanapindisha maana ya Kufufuliwa na kundi la pili wanapindisha maana ya majina na sifa za Allaah. Kundi la kwanza wanapindisha dalili za Kufufuliwa kwa sababu ya shubuha zilizowazuia kuzithibitisha, kundi la pili wanapindisha maana ya majina na sifa kwa sababu ya shubuha zilizowazuia kuzithibitisha.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 245-248
  • Imechapishwa: 20/07/2026