148. Mtazamo wa Baatwiniyyah juu ya ´Aqiydah na matendo

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kundi lingine linasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyajua mambo hayo lakini hakuyabainisha. Kwa mujibu wao wanaona kuwa aliamua kuzungumza mambo yanayopingana nayo na akataka viumbe wafahamu yale yanayopingana nayo, kwa sababu manufaa ya viumbe yanafikiwa kwa ´Aqiydah hii inayotofautiana na haki. Aidha wanasema kuwa ni lazima kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalingania watu katika itikadi ya kiwiliwili (التجسيم), licha ya kuwa ni batili, na kwamba watu wa Peponi watakula na kunywa, licha ya kuwa ni batili pia. Haiwezekani kuwalingania watu kwa njia nyingine zaidi ya hii ambayo imebeba uwongo kwa ajili ya manufaa ya viumbe. Hii ndio ´Aqiydah yao kuhusu kumuamini Allaah na siku ya Mwisho.

Kuhusu matendo, wako ambao wanayathibitisha na wengine wanaona kuwa yanawalazimu wale watu wa kawaida na si wale wasomi. Haya ni maoni ya Baatwiyyah wakanamungu, Ismaa´iyliyyah na wengineo.

MAELEZO

Wanaita kumthibitishia Allaah sifa kuwa ni kiwiliwili, kwa sababu wao wanaona kuwa sifa haziwezi kuwepo isipokuwa katika mwili. Hivyo wanadai mwenye kumthibitishia Allaah sifa amemfanya kuwa na kiwiliwili. Lakini Ahl-us-Sunnah wanasema istilahi hii haikutajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah, si kwa kuthibitishwa wala kukanushwa.

Pia wanasema hakuna kufufuliwa baada ya kufa. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizungumzia kufufuliwa kwa ajili ya kuwazuia watu na tabia mbaya. Kwa maana nyingine aliwadanganya kwa njia ya kuwatisha. Wanasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya haya kwa ajili ya maslahi ya viumbe, kwa sababu haiwezekani kuwalingania watu isipokuwa kwa njia ya kufikirisha. Ndiyo maana akatumia usulubu huo. Yale yaliyotangulia kuhusu wao ni katika mambo ya ´Aqiydah.

Ama inapokuja katika mambo ya matendo, baadhi yao wanakanusha swalah, swawm, hajj na ´ibaadah nyenginezo. Wengine wanayathibitisha kwa ajili ya watu wa kawaida. Ama wale watu wao maalum hawahitaji kufanya ´ibaadah. Ndiyo maana wale Suufiyyah waliopinduka mipaka hawafungi, hawaswali wala hawahiji. Bali hawaharamishi kitu. Bali wanahalalisha mambo ya haramu na wanasema halali na haramu ni kwa watu wa kawaida. Ama wale watu maalum hawana halali wala haramu, kwa sababu wameijua haki na hawahitaji halali na haramu. Kwa mtazamo wao watu maalum ni wale mawalii na wale nguzo ambao wameshafika kwa Allaah. Kwa hiyo kwao hawahitaji Mitume, hawahitaji Shari´ah, wala hawaharamishiwi kitu chochote na hawawajibikiwi jambo lolote.

Ismaa´iyliyyah wameitwa hivyo kwa nisba ya Ismaa´iyl bin Jafar. Kwa sababu maimamu wa Shiy´ah wanajulikana. Miongoni mwao akiwa Jafar as-Swaadiq ambaye alikuwa na watoto wawili: Muusa al-Kaadhwim bin Ja´far as-Swaadiq na Ismaa´iyl bin Ja´far. Ismaa´iyl alikufa kabla ya baba yake, lakini Muusa al-Kaadhwim aliishi baada ya baba yake. Hivyo kwa mujibu wa Ja´fariyyah uongozi ulihamia kwake na wafuasi wake wakaitwa Muusawiyyah na Ja´fariyyah. Kundi jengine wakadai kuwa Ismaa´iyl ndiye mkubwa na hivyo uongozi ulihamia kwake kutoka kwa baba yake, kwa sababu yeye ndiye alikuwa mkubwa. Ndiyo maana wakaitwa Ismaa´iyliyyah.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 242-245
  • Imechapishwa: 20/07/2026