13 – Kuvunja mifupa yake. Dalili ya hilo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika kuvunja mfupa wa muumini akiwa maiti ni kama kuvunja akiwa hai.”

Ameipokea Abu Daawuud (2/69), Ibn Maajah (1/492), at-Twahaawiy katika “al-Mushkil” (2/108), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (na. 776 – Mawaard), Ibn-ul-Jaaruud katika “al-Muntaqaa´”, uk. 551, ad-Daaraqutwniy katika “as-Sunan” yake (367), al-Bayhaqiy (4/58) na Ahmad (6/58, 105, 168, 200, 264) ambaye tamko ni lake, na Abu Nu´aym katika “al-Hilyah” (7/95), al-Khatwiyb katika “Taariykh Baghdaad” (12/106, 13:120) kupitia njia mbalimbali, kutoka kwa ´Amrah, kutoka kwake.

Baadhi ya njia zake ni Swahiyh kwa sharti za Muslim. an-Nawawiy ameitia nguvu katika “al-Majmuu´” (5/300). Ibn-ul-Qattwaan akasema: ”Cheni yake ya wapokezi ni nzuri”, kama ilivyokuja katika “al-Mirqaah” (2/380). Inayo njia mbili nyingine kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Ya kwanza iko kwa Ahmad (6/100) na nyingine iko kwa ad-Daaraqutwniy (367). Kuna nyingine yenye kuiunga mkono kutoka katika Hadiyth ya Umm Salamah ambayo ameipokea Ibn Maajah[1] na akaongeza mwishoni mwake:

“… katika dhambi.”

Hata hivyo cheni yake ya wapokezi ni dhaifu. Nayo imo katika baadhi ya njia za ad-Daaraqutwniy katika Hadiyth ya mwanzo kutoka upande wa kwanza. Lakini dhahiri ni kwamba ziada hiyo imechomekwa ndani ya Hadiyth, kwani kuna riwaya nyingine nayo kwa tamko lisemalo:

“Kwa maana katika dhambi.”

Hili ni dhahiri kwamba ziada hiyo si sehemu ya Hadiyth, bali ni tafsiri ya baadhi ya wapokezi. Hili linaungwa mkono na riwaya ya Ahmad kwa tamko lisemalo:

“Akasema: ”Wanaona kuwa hiyo ni katika dhambi.”

´Abdur-Razzaaq  amesema:

”Nadhani hayo ni maneno ya Daawuud.”

Kwa maana Daawuud bin Qays ambaye ndiye Shaykh wa ´Abdur-Razzaaq katika Hadiyth hiyo. Dhahiri ni kwamba tafsiri hiyo ndiyo inayokusudiwa katika Hadiyth. at-Twahaawiy amethibitisha hilo na akaiwekea mlango maalum katika “al-Mushkil” yake. Hivyo arejee huko anayetaka.

Hadiyth hii ni dalili ya uharamu wa kuvunja mfupa wa maiti muumini. Kwa sababu hii ikatajwa ndani ya vitabu vya Hanaabilah:

“Ni haramu kukata kiungo chochote cha mfu, kuharibu mwili wake na kumchoma moto, hata kama ameusia kufanywa hivo.”

Imetajwa namna hiyo katika “Kashshaaf-ul-Qinaa´” (2/127) na kama hivyo katika madhehebu mengine yote. Bali Ibn Hajar al-Fiqihiy amethibitisha katika “az-Zawaajir” (1/134) ya kwamba ni katika madhambi makubwa. Amesema:

“Kwa sababu imejulikana kutoka katika Hadiyth kwamba hilo ni sawa na kuvunja mfupa wa aliye hai.”

Hanaabilah wameenda mbali zaidi katika hilo mpaka wakasema, kama ilivyo katika “al-Kashshaaf” (2/130):

“Mwanamke akiwa mjamzito na inaaminika mtoto wake anaweza kuishi, basi ni haramu kupasua tumbo lake kwa ajili ya mtoto huyo, awe muislamu au kafiri mwenye mkataba wa amani, kwa sababu ndani yake kuna kuvunja heshima ya maiti aliyethibitika kufa kwa ajili ya maisha yasiyo na uhakika. Kwa sababu mara nyingi ni kwamba mtoto huyo haishi. Ahmad alitoa hoja kwa hilo katika riwaya ya Abu Daawuud kwa yaliyopokewa kutoka kwa ´Aaishah…”

Kisha akataja Hadiyth hiyo na matini ya Abu Daawuud katika “al-Masaa-il”, uk. 150:

“Nimemsikia Ahmad akiulizwa kuhusu mwanamke anayekufa na mtoto anacheza tumboni mwake. Je, apasuliwe?” Akasema: ”Hapana.” Kuvunja mfupa wa maiti ni sawa na kuvunja akiwa hai.”

Sayyid Muhammad Rashiyd Ridhwaa ameyatolea maelezo kwa kusema:

“Kutumia hoja Hadiyth hiyo kwa kuacha kumtoa mtoto hai ndani ya tumbo la mama yake hadi afe ni jambo la ajabu kwa nyanja mbili: Ya kwanza ni kwamba kupasua tumbo si kuvunja mfupa wa mfu. Ya pili ni kwamba mtoto akiwa ameumbika vizuri na akatolewa tumboni kwa kumpasua, anaweza kuishi kama ilivyotokea mara nyingi. Basi hapa tunaokoa maisha yake na tunahifadhi heshima ya mama yake kwa kuzingatia kuwa kupasua tumbo ni kama kuvunja mfupa. Hapana shaka yoyote kwamba hili la pili ndilo lenye nguvu zaidi na kwamba kupasua tumbo kwa sababu kama hii hakuzingatiwi kuwa ni kumdhalilisha maiti, kama ilivyo dhahiri kwa watu wote. Sahihi ni maoni ya wale wanaosema kuwa ni wajibu kupasua tumbo na kumtoa mtoto kama daktari ataona kuwa kuna matarajio ya maisha yake baada ya kutolewa, jambo ambalo limeelezwa wazi na baadhi yao.”

Akasema katika “Manaar-us-Sabiyl” (1/178):

“Mtoto akitoka sehemu yake akiwa hai, basi apasuliwe kwa ajili ya sehemu iliyobaki kwa kuwa maisha yake yamekuwa yakini baada ya kuwa ya dhana tu.”

Alilolichagua Sayyid (Rahimahu Allaah) ndilo sahihi kwa mujibu wa ash-Shaafi´iyyah, kama alivyosema an-Nawawiy (5/301) na akaihusisha kuwa ndio maoni ya Abu Haniyfah na wanazuoni wengi. Aidha ndio madhehebu ya Ibn Hazm (5/166-167) na hili ndilo lililo sahihi kwa idhini ya Allaah (Ta´ala).

[1] Aliihusisha katika “al-Imaam ” na akaijibu, kama ilivyo katika “Faydhw-ul-Qadiyr” na “al-Imam”. Ni kitabu muhimu sana juu ya hukumu cha Ibn Daqiyq al-´Iyd. adh-Dhahabiy amesema: “Lau kingekusanywa kwa ukamilifu na kuhaririwa, basi kingefikia juzu kumi na tano.”

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 295-297
  • Imechapishwa: 13/08/2026