Kwa kumalizia ni kwamba maneno ya Abu Muhammad al-Juwayniy ash-Shaafi´iy na wengineo kwamba ni haramu kusafiri kwa lengo la kufika sehemu tukufu yoyote isiyo ile misikiti mitatu ndiyo inapaswa kufanyiwa kazi. Kwa hivyo haishangazi kuona kwamba wanazuoni wakubwa waliobobea na wanaojulikana kwa uadilifu wao katika kufahamu dini ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayh wa sallam) waliichagua maoni hayo – mfano wa Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na Ibn al-Qayyim – Allaah awarehemu. Wao wameandika tafiti nyingi zenye manufaa katika suala hili muhimu. Miongoni mwa wanazuoni hao ni Shaykh Waliyyullaah ad-Dahlawiy. Amesema katika “al-Hujjah al-Baalighah” (1/192):

“Watu wa zama za kabla ya kuja Uislamu walikuwa wakienda sehemu walizoziaminisha kuwa ni tukufu kwa lengo la kutembelea na kutafuta baraka. Ndani ya hilo kuna upotofu mwingi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh wa sallam) akakataza upotofu huo ili watu wasichanganye kati ya ´ibaadah halisi na mambo yasiyo ya ´ibaadah, na ili hilo lisije likawa njia ya kuwaabudia wasiokuwa Allaah. Kwa mtazamo wangu haki ni kwamba kaburi, sehemu ya ´ibaadah ya mtu mwema na mlima Twur, vyote vinaingia katika katazo hili kwa usawa.”

Ni vizuri kutaja katika hitimisho hili kuwa katazo hili halihusishi kusafari kwa ajili ya biashara au kutafuta elimu, kwa kuwa safari hiyo inalenga mahitaji hayo siyo sehemu yenyewe maalum. Vivyo hivyo kusafari kwa ajili ya kumtembelea ndugu katika dini, hiyo inaruhusiwa kwani yeye ndiye anakusudiwa, kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah katika “Majmuu´-ul-Fataawaa” (2/186).

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 294-295
  • Imechapishwa: 13/08/2026