Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Wanajua pia kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewabainishia watu mambo yanayohusiana na kumuamini Allaah na siku ya Mwisho. Kumwamini Allaah na siku ya Mwisho kunajumuisha kuamini Kuanza na Kufufuliwa. Allaah ameyakusanya yote mawili pale aliposema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Na miongoni mwa watu wako wasemao: ”Tumemuamini Allaah na Siku ya Mwisho”, hali ya kuwa si wenye kuamini.”[1]

مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ

“Hakukuwa kuumbwa kwenu na wala kufufuliwa kwenu isipokuwa ni kama nafsi moja tu.”[2]

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ

”Naye ndiye aliyeanzisha uumbaji, kisha anaurudisha, nayo ni mepesi mno Kwake.”[3]

Yale ambayo Allaah (Ta´ala) ameyabainisha kuhusu kumuamini Yeye na siku ya Mwisho kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale yanayotosha kuwaongoza waja Wake na malengo Yake kubainika.

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwabainishia watu mambo ya dini yao na ´Aqiydah yao. Aliwabainishia kumuamini Allaah, kuwaamini Malaika, Vitabu, Mitume, siku ya Mwisho na kuamini makadirio kheri yake na shari yake. Aliwabainishia nguzo za imani na nguzo za Uislamu na akawabainishia matawi ya imani kwa ubainifu mkamilifu na wenye kutosha. Basi inawezekanaje auache mlango wa majina na sifa za Allaah bila kuubainisha hali ya kuwa amelibainishia ummah wake kila kitu? Nguzo za imani ni sita. Katika hizo ni kumuamini Allaah na kuiamini siku ya Mwisho. Wakati mwingine hutajwa nguzo zote za imani na wakati mwingine hutajwa kumuamini Allaah na siku ya Mwisho pekee, kwa sababu kumuamini Allaah kunapelekea kuamini mwanzo wa viumbe na kuamini siku ya Mwisho kunapelekea kuamini kufufuliwa. Mwanzo ni kule kuumbwa kwa viumbe kutoka kutokuwepo na marejeo ni kurudishwa viumbe siku ya Qiyaamah baada ya kufa. Kumetajwa kumwamini Allaah na siku ya Mwisho kwa sababu kumuamini Allaah kunapelekea kuamini mwanzo na marejeo:

مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ

“Hakukuwa kuumbwa kwenu na wala kufufuliwa kwenu isipokuwa ni kama nafsi moja tu.”[4]

Kuumbwa kwenu mwanzo na kufufuliwa kwenu baada ya kufa ni kama nafsi moja. Yule mwenye uwezo wa kuumba nafsi moja na kuirudisha ana uwezo wa kuwaumba watu wote na kuwarudisha wote. Hakuna kinachomshinda. Hakuna tofauti baina ya uwezo Wake juu ya nafsi moja na uwezo Wake juu ya nafsi zote.

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ

”Naye ndiye aliyeanzisha uumbaji… “

Huku ni kuamini mwanzo wa kuumbwa viumbe.

ثُمَّ يُعِيدُهُ

”… kisha anaurudisha… “

Huku ni kuamini siku ya Qiyaamah.

وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ

“… nayo ni mepesi mno Kwake.”

Bi maana kwa mtazamo wa akili za watu. Vinginevyo kwa Allaah vitu vyote ni vyepesi. Hakuna kinachomshinda. Lakini hii ni katika namna ya kuwashusha katika ufahamu wao; kwamba mwenye uwezo wa kuanzisha basi ana uwezo zaidi wa kurudisha.

Allaah (´Azza wa Jall) amebainisha kumwamini Allaah na kumwamini siku ya Mwisho katika Aayah nyingi ambazo kwa hizo amewaongoza waja Wake na kuwabainishia anachoksuudia. Katika kumuamini Allaah ni kuamini majina na sifa za Allaah. Katika hili kuna hoja dhidi ya wale wanaodhani kuwa Maandiko hayaleti elimu katika majina na sifa za Allaah. Kwa sababu kwa mujibu wao wanaona kuwa ni dalili za kudhaniwa tu. Ama akili kwa mujibu wao ndio dalili za yakini. Lililo wajibu ni kinyume chake; kwamba Maandiko ndio ya yakini na akili ni za kudhaniwa.

[1] 2:8

[2] 31:28

[3] 30:27

[4] 31:28

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 231-233
  • Imechapishwa: 16/07/2026