Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

113 – Imani ni moja na waumini msingi wao wanalingana katika imani hiyo.

MAELEZO

Hili ni kosa. Imani sio moja. Waumini hawalingani katika imani zao. Bali inatofautiana, inapanda na inashuka. Isipokuwa tu Murji-ah ndio wanaonelea tofauti. Hata katika kusadikisha moyoni watu hawalingani. Imani ya Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) hailingani na imani ya mtenda madhambi zaidi katika waislamu. Muislamu muovu zaidi imani yake ni dhaifu mno, ilihali imani ya Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) inalingana na imani ya ummah mzima. Kwa hivyo watu hawalingani katika imani zao.

Hata katika matendo hawalingani. Watu wanatofautiana katika matendo. Allaah (Ta´ala) amesema:

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ

“Kisha Tukawarithisha Kitabu wale tuliowateuwa miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni aliyedhulumu nafsi yake.”

Huyu ni mtenda dhambi ambaye dhambi zake ziko chini ya shirki. Ni mwenye kuidhulumu nafsi yake kwa sababu ameiweka nafsi yake khatarini:

وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ

“… na miongoni mwao aliyekuwa kati… “

Huyu ni yule anayefanyia kazi mambo ya wajibu na anajiepusha na mambo ya haramu:

وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“… na miongoni mwao aliyetangulia kwa mambo ya kheri kwa idhini ya Allaah.”[1]

Huyu ni yule ambaye anafanyia kazi mambo ya wajibu na mambo yanayopendeza na anajiepusha na mambo ya haramu, mambo yanayochukiza na baadhi ya mambo yaliyoruhusiwa kwa sababu ya kuchukua tahadhari zaidi. Ummah haulingani. Kwa hivyo makundi yamegawanyika matatu:

1 – Yule ambaye ameidhulumu nafsi yake.

2 – Yule ambaye yuko kati na kati.

3 –Yule ambaye amewatangulia wengine katika kufanya kheri.

Kwa hivyo ikajulisha kuwa imani inatofautiana.

[1]35:32-33

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 149-151
  • Imechapishwa: 19/11/2024