Wanazuoni wametofautiana kama inawajibika kwa kila siku kutia nia au inatosha kutia nia moja mwanzoni mwa Ramadhaan? Kuna maoni mbili:

1 – Inamtosheleza mfungaji kutia nia moja kwa ajili ya mwezi mzima muda wa kuwa hajakata swawm yake kwa sababu ya safari au maradhi. Haya ndio maoni ya Maalik, Ishaaq na mapokezi kutoka kwa Ahmad[1]. Hoja ni kwamba kufunga mwezi mzima ni ´ibaadah moja isiyoweza kuepukika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”… na kila mtu atalipwa kutokana na vile alivyonuia.”

Huyu amenuia kufunga mwezi na kufululiza. Kwa hivyo analipwa vile alivyonuia.

2 –  Mfungaji analazimika kutia nia tofauti kwa ajili ya kila siku. Haya ni maoni ya Abu Haniyfah, ash-Shaafi’iy na Ahmad katika maoni yaliyotangaa kwake[2]. Wamejengea hoja kwa Hadiyth ya mlango inayosema:

”… kabla ya alfajiri hana swawm.”

na:

“Yule asiyelaza nia… “

Dhahiri ya hilo ni kwamba kila usiku unahitaji nia tofauti. Kwa sababu swawm ya kila siku ni ´ibaadah inayojitegemea. Kinchojulisha hilo ni kwamba kuharibika kwa swawm baadhi ya siku za mwezi hakuharibu nyingine na kwa sababu katikati ya siku za kufunga mwezi kuna mambo yanayokinzana nayo, kwani usiku inaruhusiwa kula, kunywa na kujamii.

Matokeo ya makinzano yanadhihiri kwa yule aliyelala baada ya alasiri katika Ramadhaani na hakuamka isipokuwa baada ya kuchomoza alfajiri ya kesho. Kulingana na maoni ya kwanza ni kwamba funga yake ya siku hiyo ni sahihi, kwa sababu nia ya kwanza mwanzoni mwa mwezi inatosha. Msingi ni kuendelea kwake. Kulingana na maoni ya pili ni kwamba funga yake si sahihi, kwa sababu hakulaza nia ya kufunga siku hiyo katika sehemu ya usiku – na Allaah ndiye mjuzi zaidi[3].

[1] “al-Istidhkaar” (10/35) na “al-Mughniy” (04/337).

[2] “al-Hidayah” (01/118), “al-Mughniy” (04/337) na “al-Majmuu’” (06/302).

[3] Tazama ”Sharh-ul-Mumtiy´” (6/370).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/20-21)
  • Imechapishwa: 04/02/2025