14. Josho la lazima kabla ya ijumaa linamtosheleza mtu kwa ajili ya swalah ya ijumaa?

Swali 14: Je, josho la lazima kabla ya swalah ya Fajr linatosha kwa ajili ya swalah ya ijumaa[1]?

Jibu: Sunnah ni kuoga siku ya ijumaa wakati wa kujiandaa kwa ajili ya swalah ya ijumaa. Bora ni mtu afanye hivo wakati anapotaka kuelekea msikitini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakapokwenda mmoja wenu ijumaa basi akoge.”

Inamtosha akiwa ameoga mwanzoni mwa mchana. Kwa sababu josho la siku ya ijumaa ni Sunnah iliyokokotezwa. Wanazuoni wengine wameona kuwa ni lazima. Kwa hivyo inatakikana kuchunga josho hili siku ya ijumaa katika siku ya ijumaa. Bora mtu aoge pale anapotaka kuelekea ijumaa, kama tulivyotangulia kutaja. Kwa sababu hivi ndivo juu zaidi katika usafi na juu zaidi katika kuondosha ile harufu mbaya. Sambamba na hilo mtu atilie umuhimu manukato na mavazi mazuri.

Vivyo hivyo anatakiwa pindi anapoiendea basi atilie umuhimu unyenyekevu na akurubie kati ya hatua zake. Hatua inaondosha makosa na Allaah ananyanyua kwazo daraja. Kwa hivyo anatakiwa kuwa na unyenyekevu na kutilia umuhimu.

Anapofika msikitini basi aanze kuingia kwa mguu wake wa kulia na amswalie Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na amtaje Allaah na aseme:

أعوذ بالله العظيم وبوجهه الكريم وسلطانه القديم من الشيطان الرجيم، اللهم افتح لي أبواب رحمتك

“Najilinda kwa Allaah ambaye ni Mkubwa, kwa uso Wake mtukufu na kwa ufalme Wake wa kale kutokamana na shaytwaan aliyewekwa mbali na rehema. Ee Allaah! Nifungulie milango ya rehema Zako.”

Kisha aswali kile ambacho Allaah amemwandikia. Asijipenyeze kati ya watu wawili. Baada ya hapo aketi na asubiri ima katika kisomo cha Qur-aan, Dhikr, kumwomba Allaah msamaha au anyamaze mpaka atakapokuja imamu. Anatakiwa kunyamaza pindi imamu atapokuwa anatoa Khutbah. Kisha aswali pamoja naye. Akifanya hivo basi amefanya kheri kubwa. Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Yeyote atakayeoga kisha akaja ijumaa na akaswali kile alichoandikiwa kisha akanyamaza kumsikiliza Khatwiyb mpaka atapomaliza Khutbah yake halafu akaswali pamoja naye, basi atasamehewa yaliyo kati yake [ijumaa hiyo] na kati ya swalah nyingine ya ijumaa na ukiongezea siku tatu.”[2]

Hivyo ni kwa sababu jema moja linalipwa mara kumi mfano wake.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/404-405).

[2] Muslim (1418) na tamko lake na at-Tirmidhiy (458).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 52-54
  • Imechapishwa: 27/11/2021