Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ama jibu la kina

Kwa hakika maadui wa Allaah wana vipingamizi vingi dhidi ya dini ya Mitume [vipingamizi] ambavyo wanawazuia kwavyo watu. Katika maneno yao ni pamoja na kusema kwao: “Sisi hatumshirikishi Allaah, bali sisi tunashuhudia ya kwamba hakuna mwenye kuumba, wala hakuna mwenye kuruzuku, wala hakuna mwenye kunufaisha na kudhuru isipokuwa Allaah Mmoja pekee hali ya kuwa hana mshirika, na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamiliki katika nafsi yake si manufaa wala madhara, tusiseme ´Abdul-Qaadir au mwengine yeyote. Lakini mimi ni mwenye kufanya madhambi na hawa watu wema wana jaha mbele ya Allaah na hivyo ninamuomba Allaah kwa kupitia kwao. Mjibu kwa yaliyotangulia, nayo ni: “Wale ambao Mtume wa Allaah aliwapiga vita walikuwa wanakubali hayo uliyoyataja na walikuwa wakikubali ya kwamba waungu wao wa batili hawaendeshi kitu, isipokuwa tu walichokuwa wanataka ni jaha na uombezi.”

Msomee aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake na akayaweka wazi. Akikwambia: “Aayah hizi ziliteremshwa kwa wale waliokuwa wanaabudu masanamu! Vipi mtawafanya watu wema ni kama masanamu? Au vipi mtawafanya Mitume ni kama masanamu?” Mjibu kama ilivyotangulia. Hivyo, ikiwa atakubali ya kwamba makafiri wanashuhudia kuwa Rubuubiyyah yote ni ya Allaah, na kwamba hawakutaka chochote kutoka kwao zaidi isipokuwa uombezi tu, lakini anachotaka ni kutofautisha baina ya kitendo chao na kitendo chake kwa aliyoyataja, mkumbushe ya kwamba miongoni mwa makafiri kulikuwa wanaoabudu masanamu, watu wema na masanamu, wengine wakiwaabudu mawalii.

Allaah amesema kuhusu wao:

أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

”Hao wanaowaomba wao wenyewe wanatafuta kwa Mola wao njia ya kujikurubisha na kujikurubisha Kwake kadri na wanavyoweza.” (al-Israa´ 17 : 57)

Na wanamuomba ´Iysa bin Maryam na mama yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ ۖ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ ۗ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمُ الْآيَاتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ  قُلْ أَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا ۚ وَاللَّـهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

”al-Masiyh, mwana wa Maryam, si chochote isipokuwa ni Mtume tu, bila shaka wamekwishapita kabla yake Mitume wengine na mama yake alikuwa mkweli sana. Wote wawili walikuwa wanakula. Tazama jinsi Tunavyowabainishia Aayah – kisha tazama vipi wanavyogeuzwa!” Sema: “Vipi mnaabudu asiyekuwa Allaah asiyemiliki kukudhuruni wala kukunufaisheni? Allaah ndiye Mwenye kusikia yot, Mjuzi wa yote.” (al-Maaidah 05 : 75- 76)

Mtajie Kauli Yake (Ta´ala):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

”Na siku Atakayowakusanya wote kisha atawaambia Malaika: “Je, hawa ndio waliokuwa wakikuabuduni nyinyi?” Watasema: “Umetakasika! Wewe ndiye Mlinzi wetu na tunajitena mbali na wao. Bali walikuwa wakiabudu majini ambao wengi wao wakiwaamini.” (Saba´ 34 : 40-41)

Na Kauli Yake (Ta´ala):

إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ

”Na Allaah atakaposema: “Ee ‘Iysaa, mwana wa Maryam! Je, wewe ndiye uliwaambia watu: “Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu miwili badala ya Allaah?” Atasema: “Utakaso ni Wako! Vipi nitasema yale yasiyo kuwa haki kwangu? ikiwa nimesema hayo basi Ungeliyajua. Unayajua yale yote yaliyomo ndani ya nafsi yangu na wala mimi sijui yale yaliyomo ndani ya Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi yote yaliyojificha.”” (al-Maaidah 05 : 116)

Mwambie: “Umejua sasa ya kwamba Allaah amemkufurisha yule aliyeyaabudu masanamu na watu wema na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawapiga vita?”

Ikiwa atasema: “Makafiri walikuwa wanataka [manufaa na madhara] kutoka kwao ilihali mimi ninashuhudia ya kwamba Allaah ndiye Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru na Mwendeshaji wa mambo. Sitaki [manufaa na madhara] isipokuwa tu kutoka Kwake. Watu wema hawana katika hilo lolote, lakini ninawaomba kwa kuwa natarajia kutoka kwa Allaah uombezi wao.” Jibu ni kuwa, maneno haya na yale ya makafiri ni sawa sawa. Msomee Kauli Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah karibu.”” (az-Zumar 39 : 03)

Kauli Yake (Ta´ala):

وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (Yuunus 10 : 18)

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) ameanza kwa jibu la kijumla, kama ilivyotangulia, kisha jibu la kina. Anawajibu watu wenye utata kwa jibu la kijumla na jibu la kupambanua. Kwa sababu watu wa shubuha wamegawanyika aina mbili:

1 – Wako ambao wanaelewa mapema wanahitajia kupambanuliwa.

2 – Wako wengine ambao ni wajinga na inamtosha kwake kumjibu kwa jumla.

Kinacholengwa ni kwamba maadui wa Allaah katika washirikina wana shubuha ambazo wanazitumia kutaka kuwapaka watu mchanga wa machoni dhidi ya dini ya Mitume. Kwa ajili hii ndio maana akataja jibu la kina ambalo linatumika kama Radd kwa washirikina. Wakisema eti tusiwafanye kama makafiri wale wa mwanzo waliokuwa wakiyaabudu masanamu na kwamba wao hawayaabudu masanamu na kwamba eti wanafanya Tawassul kwa waja wema, Mitume na watu wema. Mweleze kuwa yeye amefanya yaleyale yaliyofanywa na wao. Wao hawakuyaabudu masanamu peke yao. Waliyaabudu masanamu, Mitume, waja wema, al-Laat ambaye alikuwa mja mwema, ´Iysaa na mama yake, ambapo ´Iysaa alikuwa Mtume na mama yake alikuwa mja mwema, waliwaabudu mawalii na waja wengine wema. Kwa hiyo hakuna tofauti. Akisema kwamba yeye hamshirikishi Allaah na chochote na kwamba anakiri kuwa Allaah ndiye Muumbaji, Mruzuku, Mwenye kuyaendesha mambo, Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha. Lakini kwamba anafanya hivo kwa sababu ya kutaka uombezi kutoka kwao na kwamba anafanya Tawassul kupitia wao ili wamkurubishe mbele ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Mweleze kwamba hiyo ndio dini ya washirikina. Kama unataka kufuata haki basi mwabudu na umuombe Allaah pekee na kwamba asiyaombe masanamu, Mitume wala waja wema. Ni mamoja mtu akamuomba Mtume, mja mwema, sanamu au mti. Yote hayo ni kumshirikisha Allaah na wala haifai. Wakiwa ni waja wema na ni Mitume, basi wema ni wa kwao na si wako. Lakini kufanya Tawassul kunakuwa kwa matendo mema. Unatakiwa kuwaiga; swali kama wanavyoswali, funga kama wanavyofunga, mtakasie Allaah ´ibaadah kama wao wanavyomtakasia, amrisha mema kama wao wanavyoamrisha mema, kataza maovu kama wao wanavyokataza. Hivi ndivo kuwaiga. Fanya kama wanavofanya wao matendo mema. Ama kuwaomba pamoja na Allaah kama mfano wa kusema “Ee Mtume wa Allaah! Ninisuru! Mponye mgonjwa wangu! Ee Bwana ´Abdul-Qaadir! Ee Ahmad al-Badawiy! Ee al-Husayn! Ee al-Hasan! Ee ´Aliy!” Unawaomba kisha unasema eti huwaabudu na kwamba unawaomba kwa sababu ni waja wema na kwamba ni Mitume. Hii ndio ´ibaadah ileile iliokuwa ikifanywa na Abu Jahl, ´Utbah bin Rabiy´ah na makafiri wengine mfano wao wa Quraysh. Hii ndio dini yao ambao Allaah ametueleza kwamba wamesema:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah karibu.”[1]

Hatuwaabudu kwa sababu eti wanaumba au wanaruzuku. Wanasema kuwa wanawaabudu ili wawakurubishe mbele ya Allaah. Amesema (Ta´ala) juu yao:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[2]

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi haitowafaa uombezi wowote wa waombezi.”[3]

Kwa sababu wameiomba kinyume na njia yake. Yule mwenye kutaka uombezi basi amuombe nao Allaah na awafanye Mitume na waja Wake wengine wema waweze kumuombea. Anatakiwa kufuata njia yao na amwabudu Allaah kama walivyomwabudu, amuombe Allaah kama alivyomuomba, amtake msaada Allaah kama wao walivyomtaka. Anatakiwa kufuata mfumo wao katika kumwabudu Allaah pekee, kutii maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Ama kuwaomba wao pamoja na Allaah, akawataka msaada, akawawekea nadhiri na akatufu kwenye makaburi yao. Matendo haya ndio shirki yenyewe waliokuwa wakifanya washirikina wa kale. Hii ndio dini ya wale wa mwanzo. Dini ya washirikina ilikuwa kujikurubisha mbele ya Allaah kwa kuwaabudu waja wema, kuwafanya wakati na kati kwa njia ya kwamba wakawaomba pamoja na Allaah na kuwataka uokozi kwa madai eti:

هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”

Ni yaleyale yaliyosemwa na wale wa mwanzo. Amesema (Ta´ala):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

“Siku atakayowakusanya wote kisha atawaambia Malaika: “Je, hawa  ndio waliokuwa wakikuabuduni?” Watasema: “Utakasifu ni Wako!” Wewe ni mlinzi badala yao! Bali walikuwa wakiabudu majini, wengi wao wakiwaamini.”[4]

 وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ

“Ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayemwomba badala ya Allaah, ambao hatowaitikia mpaka siku ya Qiyaamah nao hawatambui maombi yao.”[5]

Ni wenye kughafilika juu ya maombi yao:

وَإِذَا حُشِرَ النَّاسُ

“Wakati watakapokusanywa watu… “

Bi maana watu wote:

كَانُوا لَهُمْ أَعْدَاءً وَكَانُوا بِعِبَادَتِهِمْ كَافِرِينَ

“… [waungu wao] watakuwa ni maadui wao, na watakuwa wenye kuzikanusha ‘ibaadah zao.”[6]

Amesema kuhusu wale wenye kumwabudu al-Masiyh na mama yake na waja wengine wema:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ

“Hao wanaowaomba… “

Bi maana wale ambao washirikina wanawaomba:

يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ

“… [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia… “

Wao wenyewe wanatafuta kwa Mola wao njia:

أَيُّهُمْ أَقْرَبُ

“… [na] kumkurubia kadri wanavyoweza… “

Njia ni kule kujikurubisha kwa kumtii Yeye:

أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“… [na] kumkurubia kadri wanavyoweza na wanataraji rehema Zake na wanakhofu adhabu Yake.”[7]

Hii ndio hali yao ambapo wanamwabudu Allaah, wanajikurubisha Kwake, wanamukhofu na wanamtarajia ilihali wao ni Mitume na waja wema. Kwa hivyo wewe pia ukiwa ni mkweli na unataka kuwafuata, basi fanya kama wanavyofanya wao. Usiwaabudu! Kwani wao ni waja kama wewe. Ni viumbe na wenye kuruzukiwa. Hawamiliki juu yako manufaa wala madhara kama ambavyo wewe mwenyewe unalikubali hilo. Hawamiliki madhara, manufaa, kufisha, kuhuisha wala kufufua. Ikiwa hii ndio hali yao, na wewe mwenyewe unalikubali hilo, basi mwombe Allaah ambaye wao pia wanamwomba, mwabudu Allaah ambaye wao pia wanamwabudu, mfanyie nadhiri,  mchinjie Yeye, swali kwa ajili Yake, mfungie Yeye na mengineyo katika ´ibaadah wanazozifanya ili uwe kama wao, upate ujira na thawabu na kufaulu kama wao walivyofaulu. Hii ndio hali ya washirikina katika zama za mtunzi wa kitabu na katika zama zetu hii leo na hata kabla ya zama za mtunzi wa kitabu. Hii ndio hali yao. Vivyo hivyo katika zama za Quraysh, kabla ya hapo katika zama za watu wa Nuuh, Huud na Swaalih. Wote namna hii ndivo ilikuwa shirki yao. Ni mara chache mno ilikuwa utampata mtu akisema kuwa waungu wao wanaumba na kuruzuku. Hii ni shriki iliokuwa inajitokeza mara chache mno kwa sababu ni kushirikisha katika Tawhiyd-ur-Ruruubiyyah. Washirikina wengi shirki yao inakuwa katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah wakati wa kuabudu, kutafuta uokozi, kufanya Tawassul kupitia kwao kwa kuomba uombezi, kujikurubisha kwao mbele ya Allaah na kuwaomba wawaponye wagonjwa wao. Haina maana walikuwa wanaona kuwa wao wenyewe ndio wanaponya. Lakini walikuwa wanaona kuwa wanawaponya wagonjwa wao kwa sababu ya kumuomba Allaah ilihali wao wameshageuka mifupa ndani ya makaburi yao! Hakika huu ni ujinga mkubwa. Huyu ameshakuwa maiti na roho imeshatoka ndani ya kiwiliwili  chake ambaye hanufaishi manufaa wala madhara. Vipi huyu ataweza kukuombea? Vipi huyu ataweza kukusalimisha kutokamana na adhabu na maradhi eti kwa kukuombea? Hakika huu ni ujinga mkubwa. Tunamuomba Allaah afya.

[1] 39:03

[2] 10:18

[3] 74:48

[4] 34:40-41

[5] 46:05

[6] 46:06

[7] 17:57

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 45-49
  • Imechapishwa: 14/10/2021