Haafidhw ´Abdul-Ghaniy al-Maqdisiy al-Hanbaliy (Rahimahu Allaah) amesema:

188 –  ´Aaishah na Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anakutwa na alfajiri hali ya kuwa ana janaba kutokana na wake zake, kisha akaoga na kufunga.”[1]

MAELEZO

Katika Hadiyth hii ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anakutwa na alfajiri hali ya kuwa ana janaba kutokana na wake zake, kisha akaoga na kufunga.

Imekuja katika tamko la Muslim:

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anakutwa na alfajiri katika Ramadhaan hali ya kuwa ana janaba, si kwa sababu ya ndoto, kisha akaoga na kufunga.”[2]

Hadiyth hii ina faida zifuatazo:

1 – Usahihi wa kufunga kwa mwenye janaba.

2 – Inafaa kwa mwenye janaba kuchelewesha kuoga hadi baada ya alfajiri. Hapo ni pale ambapo mtu anapokuwa na janaba mwishoni mwa usiku, ni mamoja iwe kutokana na wakeze au kutokana na ndoto, vilevile mwanamke aliyemaliza hedhi au damu ya uzazi mwishoni mwa usiku na muda umekuwa mfupi kiasi kwamba hawezi kuoga na kula daku, basi akiamua kuoga huenda akakosa daku, na akila daku huenda akakutwa na alfajiri hali ya kuwa ana janaba. Hivyo basi anaanza kwa kula daku hali ya kuwa ana janaba, kisha anaoga baada ya daku yake. Hata ikifika alfajiri hali hiyo haidhuru kulingana na dhahiri ya Hadiyth hii na kufunga kwake ni sahihi. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anakutwa na alfajiri hali ya kuwa ana janaba kutokana na jimaa, si kwa sababu ya ndoto, kisha anafunga, lakini alikuwa anaharakisha kuoga ili aswali swalah ya Fajr pamoja na mkusanyiko.

[1] al-Bukhaariy (1926) na Muslim (1109).

[2] Muslim (1109).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr Dhil-In´am bisharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/443)
  • Imechapishwa: 01/03/2025